Liverpool kuzuru Porto ikilenga kufunga kazi
INGAWA watakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wao wengi; FC Porto wana mlima mrefu wa kukwea mbele ya Liverpool leo Jumatano usiku katika mechi ya marudiano ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kwenye mechi hiyo itakayochezewa ugani Estadio do Dragon jijini Porto, wenyeji wanatakiwa kubadilisha kichapo cha 2-0 walichopokea ugani Anfield katika pambano la mkondo wa kwanza.
Porto wanaingia uwanjani baada ya kuandikisha ushindi mkubwa wa 3-0 ugenini dhidi ya Portimonense katika mechi ya Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) mwishoni mwa wiki jana.
Ni ushindi ambao pamoja na ule wa Benfica dhidi ya Vitoria de Setubal unawaweka katika nafasi ya kwanza jedwalini, lakini nyuma ya Benfica walio na idadi kubwa ya mabao.
Kihistoria, Porto wanajivunia rekodi nzuri ya nyumbani baada ya kushindwa mara mbili pekee katika mechi 14 msimu huu. Vile vile, wamehifadhi rekodi ya kutofungwa nyumbani katika mechi tano kati ya saba za karibuni.
Hata hivyo, bado kuna shauku kuhusu mechi hii ya usiku kwa sababu vijana hao wa kocha Sergio Conceicao watakuwa wakicheza dhidi ya Liverpool inayojivunia washambuliaji matata wanaofahamu jinsi ya kutandaza soka ya Klabu Bingwa barani Ulaya.
Wakati watu wakifikiria Liverpool walipata ushindi huo kwa kubahatisha, vijana hao wa Jurgen Klopp waliichapa Chelsea 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) siku chache baadaye.
Chelsea ilitarajiwa kushinda mechi hiyo kutokana na kiwango kizuri, lakini wakashindwa kuwika huku staa wao Eden Hazard akipiga mwamba wa goli mara mbili.
Iwapo Liverpool watashinda, watasonga mbele na kukutana na Barcelona ambayo ilibeba ushindi wa 1-0 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza na kuilaza Manchester United katika mkondo wa pili.
Itafahamika kwamba Liverpool ni miongoni mwa timu tatu zilizoanza vibaya kabla ya kuimarika kwa haraka na kusonga mbele. Zingine ni Manchester United iliyoibandua PSG ya Ufaransa na Juventus iliyopiga Atletico Madrid ya Uhispania.
Porto imewahi kupoteza kwa 2-0 katika mechi za awali na kushindwa kubadilisha matokeo.
Isitoshe, Liverpool haijawahi kushindwa na Port katika mechi ya bara ambapo inajivunia ushindi mara nne na sare tatu.
Msimu uliopita, Liverpool iliitandika mabao 5-0 katika hatua ya 16 bora, lakini inakumbukwa kwamba Porto ndio tu timu inayojivunia ushindi wa asilimia 100 katika mechi za nyumbani katika michuano hii.
Walishinda mechi tano mfululizo katika mashindano tofauti ya bara Ulaya kati ya 1998 na Desemba 1999.
Liverpool imeshinda mechi nne za ugenini tangu msimu huu uanze, na kushindwa mara moja tu kwa AS Roma, na kusonga mbele licha ya matokeo hayo.