Liverpool wakabwa na West Ham United
NA MASHIRIKA
KLABU ya Liverpool imekabwa na West Ham United kwa sare ya 2-2 ugani London Stadium mnamo Jumamosi.
Liverpool wamepata mabao kupitia kwa Andrew Robertson kunako dakika ya 48 na Alfonse Areola aliyejifunga katika dakika ya 65.
Wenyeji West Ham almaarufu The Hammers, walikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 43 baada ya Jarrod Bowen kucheka na nyavu. Michail Antonio alifunga bao la pili la wenyeji katika dakika ya 77.
Sare hii inadidimiza matumaini ya Liverpool almaarufu The Reds, ambao kwa sasa wako katika nafasi ya tatu katika jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 75 baada ya mechi 35 nyuma ya Manchester City (76) na viongozi Arsenal (77).
Man City wamecheza mechi 33 nao Arsenal wamecheza mechi 34.