Michezo

Maafisa wa voliboli Misri wachunguzwa

February 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

SHIRIKISHO la Voliboli Duniani (FIVB) limeanzisha uchuguzi kuhusu udanganyifu uliohusisha mashirikisho mawili uliodhamiria kuhakikisha timu ya wanawake ya Misri imefuzu kushiriki Olimpiki za mwaka huu.

FIVB inachunguza jinsi maafisa wa Shirikisho la Voliboli la Afrika (CAVB) na lile la Voliboli nchini Misri walivyoruhusu mchezaji wa Misri, Farida El Askalany kushiriki mashindano mawili kwa wakati mmoja.

Kisa hicho kilishuhudiwa kwenye mashindano ya voliboli ya kawaida (indoor) na voliboli ya ufukweni yaliyoandaliwa nchini Cameroon na Eritrea mtawalia.

Huenda mashirikisho hayo yakawekewa vikwazo kali na FIVB endapo yatapatikana na hatia kuhusiana na tuhuma hizo zilizogunduliwa siku ya mwisho katika voliboli ya kawaida nchini Cameroon.

Kulingana na sheria za FIVB, mchezaji anayeshiriki voliboli ya ufukweni hapaswi kushiriki voliboli ya kawaida hasa endapo mashindano yanafanyika kwa wakati mmoja.

Mchezaji huyo alikuwa akishiriki mashindano ya ufukweni nchini Eritrea yaliyokamilika tarehe 7 mwezi huu, siku mbili baada ya mechi za voliboli ya kawaida kuanza.

Huku kamati iliyoendesha mashindano hayo iliyojumuisha, Hicham Sayed wa Misri iliyohusika na udanganyifu huo ikifahamu inachofanya, mchezaji huyo alitua nchini Cameroon tarehe 6, siku moja baada ya mechi hizo kukunjua jamvi ambapo hakucheza mechi baina ya Kenya na Misri.

Hata hivyo, jina lake lilikuwepo katika fomu ya wachezaji wa kikosi cha Misri. Inadaiwa kuwa kamati hiyo ilifanya mchezo mchafu uliotoa nafasi kwa Misri kutokuwa na mechi siku ya pili ya kipute hicho ili kuhakikisha mchezaji huyo amejiunga na wenzao nchini humo. Farida aliruhusiwa kushiriki mechi ya pili ambapo Misri ilishinda Nigeria.

”Ni makosa kwa mchezaji kushiriki mashindano mawili kwa wakati mmoja,” alisema ofisa wa kikosi cha Kenya aliyejaribu kupiga hatua hiyo wakiwa nchini Cameroon lakini malalamishi yake yalipigiwa chini na maofisa wa kamati iliyosimamia kipute hicho.

Malkia Strikers ya Kenya ilitwaa tikiti ya kushiriki Olimpiki za mwaka huu jijini Tokyo, Japan baada ya kushinda wapinzani wao Misri, Nigeria, Botswana na Cameroon.

Vipusa hao chini ya kocha, Paul Bitok walikomoa Nigeria kwa seti 3-0 (25-15, 25-21, 25-12), pia walinyuka Indomitable ya Cameroon kwa seti 3-2( 25-16, 23-25, 25-21, 23-25, 15-11).

Wanakimia hao walianza kampeni zao kwa kuandikisha ushindi wa mechi mbili kwa seti 3-1 ( 25-23, 25-15, 25-21, 25-22 ) na 3-0 (25-17, 25-19, 25-19) dhidi ya Misri na Botswana mtawalia.

Ufanisi huo umewawezesha kurejea kushiriki kipute hicho baada ya miaka 16. Kenya ilikosa kushiriki kipute hicho makala ya mwaka 2008 (Uchina) 2012 (Uingereza) na 2016(Brazil).

Katika mechi ya kufuzu kwa Olimpiki mwaka 2016, Kenya ilichapa Cameroon seti 3-1 katika makundi kabla ya kuzidiwa maarifa na Misri ilipozabwa seti 3-2 katika nusu fainali.

Ndani ya miaka miwili iliyopita, Cameroon imeonekana kivingine katika voliboli ya Bara Afrika. Kwenye fainali za Kombe la Afrika mwaka 2019, Kenya ilikomoa Cameroon kwa seti 3-2 katika mechi za makundi, lakini ilipokezwa kichapo sawa na hicho katika fainali kwenye mechi zilizofanyika jijini Cairo, Misri.

Mwezi mmoja baadaye, Malkia ililipiza kisasi kwa kulaza Cameroon seti 3-1 kwenye mechi za makundi pia katika fainali ya Michezo ya Afrika (All Africa Games) mjini Rabat nchini Morocco.

Kadhalika Kenya ilinyanyua Cameroon kwa seti 3-1 kwenye mechi za kombe la dunia mwaka 2019. Kenya imewahi kushiriki michezo ya Olimpiki mara mbili mwaka 2000, iliyofanyika mjini Sydney nchini Australia pia mwaka 2005 mjini Athens nchini Ugiriki.