Michezo

Mabao 31 yavumwa siku ya mwisho ya EPL, Salah avunja rekodi

May 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

LIGI Kuu ya Uingereza imeshuhudia mabao 31 yakifungwa katika siku ya mwisho ya msimu 2017-2018, huku mabingwa Manchester City wakiweka rekodi ya alama 100, Tottenham ikimaliza mbele ya Liverpool nayo Swansea ikatupwa Ligi ya Daraja ya Pili. Mmisri Mohamed Salah ndiye mfungaji bora baada ya kutiksa nyavu mara 32 na kuvunja rekodi ya mabao 31 iliyokuwepo.

Mfungaji bora wa msimu 2015-2016 na 2016-2017 Harry Kane alifunga msimu kwa magoli 30.  

City ilivuna alama tatu dhidi ya Southampton kupitia bao la Mbrazil Gabriel Jesus zikisalia sekunde chache dakika tano za majeruhi zikamilike.

Mechi kati ya Tottenham, ambayo imeajiri Mkenya Victor Wanyama, na Leceister ilishuhudia mabao tisa. Tottenham ilitolewa kijasho na Leicester kabla ya kuishinda 5-4 kupitia mabao ya Harry Kane na Erick Lamela (mawili kila mmoja) na bao la kujifunga kutoka kwa beki wa Austria, Christian Fuchs. Leicester, ambayo ilitangulia kufunga na kutupa uongozi mara mbili kabla ya kuzimwa, ilipata mabao yake kutoka kwa Jamie Vardy (mawili), Riyad Mahrez na Kelechi Iheanacho.

Matumaini ya Liverpool kumaliza katika nafasi ya tatu yalitegemea matokeo ya mchuano huu. Kwa muda mrefu, Liverpool ilionekana itamaliza nyuma ya mabingwa City na nambari mbili Manchester United, lakini ushindi wa Spurs ukazima matumaini hayo.

Hata hivyo, Liverpool itashiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora. Ilipepeta Brighton 4-0 kupitia mabao ya wachezaji Salah, Dejan Lovren, Dominic Solanke na Andrew Robertson.

Kocha mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger alikamilisha enzi yake ya miaka 22 kwa kushinda Huddersfield 1-0 kupitia bao la Pierre-Emerick Aubameyang.

Naye kocha Antonio Conte, ambaye karibu msimu wote uvumi umekuwa ukidai atatemwa na Chelsea, alikamilisha msimu vibaya baada ya vijana wake kupapurwa 3-0 na Newcastle iliyoona lango kupitia Ayoze Perez (mabao mawili) na Dwight Gayle.

Marcus Rashford, ambaye tetesi zimekuwa zikisema hana raha uwanjani Old Trafford, alifungia Manchester United bao lililozamisha Watford 1-0.

City ya kocha Pep Guardiola, United ya Jose Mourinho, Spurs ya Mauricio Pochettino na Liverpool ya Jurgen Klopp zitapeperusha bendera ya Uingereza katika Klabu Bingwa msimu ujao. Chelsea, Arsenal na Burnley, ambazo zimekalisha msimu katika nafasi za tano, sita na saba, mtawalia, zitashiriki Ligi ya Uropa.

Swansea, Stoke na West Brom zitashiriki Ligi ya Daraja ya Pili msimu ujao. Swansea imekuwa timu ya mwisho kutemwa baada ya kulemewa 2-1 na Stoke, Jumapili. Ilikuwa inawania nafasi ya kukwepa shoka dhidi ya Southampton, ambayo ilibahatika kusalia ngazi ya juu licha ya kukomolewa 1-0 na City.

Katika matokeo mengine Jumapili, Burnley imelimwa 2-1 na Bournemouth, Crystal Palace ikazaba West Brom 2-0 na West Ham ikanyamazisha Everton 3-1.