Michezo

Mabinti wa KCB walenga taji la Afrika voliboli

February 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya voliboli ya wanawake ya KCB haina la ziada mbali inapania kushinda taji la Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka huu.

Warembo hao wanalenga kuleta kombe hilo hapa Kenya kwa mara ya kwanza tangu 2006 waliposhinda taji hilo.

Kocha mkuu wake, Japheth Munala amedokeza hayo na kutaja kuwa wamo mbioni kuunda timu imara ili kutoa upinzani propa katika ligi ya KVF pia mashindano mengine barani.

Tangu kukamilika kwa mechi za ligi msimu uliyopita uongozi wa wanabenki hao umekuwa mbioni kutafuta wachezaji wazoefu ili kujiweka pazuri kukabili wapinzani wengine muhula huu.

Tayari klabu hiyo imethibitisha kunasa huduma za wachezaji sita wapya katika harakati za kukisuka kikosi hicho.

KCB iliyomaliza ya pili katika fainali za ligi msimu uliyopita imesaini wachezaji sita wapya ambao ni kati ya mastaa ambao hupigia kikosi hicho cha taifa maarufu Malkia Strikers.

Mchezaji wa KCB, Belinda Barasa arukia mpira walipocheza na Kenya katika fainali ya Ligi Kuu ya KVF muhula huu. Picha/ John Kimwere

Benchi la kiufundi chini ya kocha wa malkia strikers, Paul Bitok tayari limetaja kuwa nimenasa huduma za nahodha wa kikosi hicho cha taifa, Mercy Moim na Sharon Chepchumba aliyetamba katika pambano la Klabu Bingwa Afrika nchini Misri msimu uliyopita.

Aidha imesajili Edith Wisa, Sharon Amito aliyekuwa akipigia Ndejje University ya Uganda. Pia wapo Sharon Sandui na Emmaculate Nekesa kutoka Shule ya Upili ya Kwanthanze.

Munala alipofanya vizuri katika kipute cha Klabu Bingwa aliongoza Pipeline kumaliza ya pili mwaka 2015 iliponyukwa seti 3-1 na Al Ahly ya Misri.

Paul Bitok ndiye kocha mkuu wa Malkia Strikers ambapo amefanikiwa kuiongoza na kutwaa tiketi ya kushiriki Olimpiki za mwaka huu.

”Nimepania kusaidia KCB kuibuka malkia wa Afrika katika voliboli pia kuifanya kati ya klabu zinazolipa wachezaji vizuri ili kujitemea,” anasema kocha, Bitok na kuongeza kuwa timu za Kenya zinastahili kuiga mtindo wa mataifa ya Kaskazini mwa Afrika.

Kocha Japheth Munala alipohamia KCB waliandamana na wachezaji wengi kutoka klabu ya Kenya Pipeline. Hatua ya kusajili wachezaji sita imechangia kukutanishwa na wenzao waliokuwa wakichezea Malkia Strikers.

Waliojiunga na kikosi hicho mapema mwaka jana walikuwa Noel Murambi, Violet Makuto, Leoninda Kasaya na Jemimah Siang’u. Pia KCB ilisajili mchezaji wa kigeni raia wa Rwanda, Ernestine Akimanizanye.

Hata hivyo tunapania kushiriki mazoezi ya pamoja ili wachezaji wapate nafasi ya kuzoeana kama kundi moja ili kuonyesha weledi wao hatua tunayoamini itawasaidia kukamata anga za kimataifa katika voliboli,” alisema kocha Munala.

Kwenye kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAVB) mwaka uliyopita, KCB ilishindwa kufana na kumaliza ya tisa kwenye jedwali.

Ilimaliza ya tisa baada ya kupepeta Revenue Authority ya Rwanda seti 3-0 pale nahodha, Noel Murambi alipoongoza wenzake kutesa wapinzani wao na kunasa ufanisi wa alama za 25-15, 25-13, 25-11.

KCB ilijikatia tiketi ya mchezo huo ilipozoa seti 3-0 (25-10, 25-15, 28-0) mbele ya USFA ya Burkina Faso. Kwenye robo fainali za kuwania tisa bora vipusa hao waliandikisha seti 3-0 mbele ya Shooting ya Misri.