Maguire aongoza kwa bei Pepe wa Arsenal akifuatia
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
KLABU za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zilimwaga karibu Sh174.7 bilioni kunyakua wachezaji 114 katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichoanza Mei 17 na kufungwa Agosti 9.
Kiasi hicho cha fedha ni Sh19.7 bilioni zaidi ya fedha zilizotumiwa katika kipindi kama hicho cha uhamisho wa mwaka 2018. Huu ni mwaka wa nne mfululizo ambapo jumla ya fedha zilizomwagwa sokoni zimepita pauni bilioni moja za Uingereza (Sh124.7 bilioni).
Mwingereza Harry Maguire alikuwa mchezaji ghali zaidi aliyenunuliwa katika kipindi hicho na pia amerukia juu ya daftari za mabeki ghali duniani alipotua Manchester United kwa Sh10 bilioni kutoka Leicester City.
Arsenal ilitumia Sh9 bilioni kusaini mshambuliaji wa Ivory Coast, Nicolas Pepe kutoka Lille, huku sajili zingine ghali zikijumuisha kiungo Mfaransa Tanguy Ndombele (Sh7.8 bilioni kutoka Lyon hadi Tottenham) na Manchester City kuajiri kiungo Mhispania Rodri (Sh7.8 bilioni kutoka Atletico Madrid) na beki Mreno Joao Cancelo (Sh7.4 bilioni kutoka Juventus).
Jinsi klabu zilitumia fedha zao sokoni: Mabingwa mara 20 wa Uingereza, Manchester United walikuwa juu ya orodha ya timu zilizotumia fedha nyingi sokoni. United ilimwaga Sh18.4 bilioni baada ya rekodi ya ada kubwa iliyotumiwa kupata Maguire iliyofuata kusajiliwa kwa beki Aaron Wan-Bissaka (Sh6.2 bilioni kutoka Crystal Palace) na kiungo wa Wales Daniel James (Sh2.2 bilioni kutoka Swansea).
Cha kustaajabisha ni kuwa Aston Villa, ambayo inarejea EPL baada ya kuwa Ligi ya Daraja ya Pili msimu mitatu, ilikaribia kuwa bega kwa bega na United juu ya jedwali ya timu zilizotumia fedha nyingi. Villa ilimwaga Sh18.0 bilioni kusaini wachezaji 12 wakiongozwa na beki Muingereza Tyrone Mings (Sh3.3 bilioni kutoka Bournemouth), mshambuliaji Mbrazil Wesley (Sh2.7 bilioni kutoka Club Brugge), beki Muingereza Matt Targett (Sh2.1 bilioni kutoka Southampton) na kiungo raia wa Brazil, Douglas Luiz (Sh1.8 bilioni kutoka Manchester City).
Sajili ghali sokoni katika kipindi kirefu cha mwaka 2019:
Arsenal ilivunja rekodi yake ya kuwa “mkono gamu” ilipomwaga Sh17.2 bilioni kwa kusajili Pepe, beki Mfaransa William Saliba (Sh3.3 bilioni kutoka Saint-Etienne na kumrejesha katika klabu hiyo kwa mkopo), beki wa Scotland Kieran Tierney (Sh3.1 bilioni kutoka Celtic), beki Mbrazil David Luiz (Sh1 bilioni kutoka Chelsea), mshambuliaji Mbrazil Gabriel Martinelli (748.4 milioni kutoka Ituano) na kumchukua kiungo Mhispania Dani Ceballos kwa mkopo kutoka Real Madrid.
Manchester City iliwekeza Sh16.8 bilioni kwa kunyakua Rodri na Joao Cancelo pamoja na kipa Mwamerika Zackary Steffen (Sh872.5 milioni kutoka Columbus Crew) na beki Mhispania Angelino Jose Angel (Sh660.7 milioni kutoka PSV Eindhoven).
Matumizi ya Everton yalikuwa Sh14.7 bilioni baada ya kununua mshambuliaji Mnigeria Alex Iwobi kutoka Arsenal pamoja na mshambuliaji Mwitaliano Moise Kean (Sh3.4 bilioni kutoka Juventus), kiungo wa Ivory Coast Jean-Phillippe Gbamin (Sh3.1 bilioni kutoka Mainz 05), kiungo Mreno Andre Gomes (Sh2.7 bilioni kutoka Barcelona) na kiungo Muingereza Fabian Delph (Sh1.1 bilioni kutoka Manchester City).
Klabu nyingine iliyopitisha pauni milioni 100 (Sh12.4 bilioni) ni Tottenham Hotspur iliyovua kiungo Muingereza Ryan Sessegnon kutoka Fulham kwa Sh3.7 bilioni. Ilikuwa imesajili Ndombele na mshambuliaji chipukizi Jack Clarke (Sh1.0 bilioni kutoka Leeds United na kumrejesha katika klabu hiyo kwa mkopo).
Spurs, ambayo bado ina kiungo Mkenya Victor Wanyama katika kikosi chake baada ya kushindwa kumuuza nchini Uingereza, inafuatiwa na Leicester (Sh11.3 bilioni), West Ham (Sh9.7 bilioni), Newcastle, Wolves (wote Sh8.1 bilioni), Brighton (Sh7.2 bilioni), Southampton (6.2 bilioni), Bournemouth (Sh5.7 bilioni) na Watford (Sh5.6 bilioni).
Mwisho kabisa kwenye orodha hii ni washiriki wapya Norwich waliotumia Sh137.1 milioni nao Liverpool walitumia Sh549 milioni, Crystal Palace (Sh1.3 bilioni), Burnley (Sh1.8 bilioni), Chelsea (Sh4.9 bilioni) na Sheffield United (Sh5.3 bilioni).