Michezo

MAHOJIANO: Sina machungu ya kupigwa teke na Kenya – Migne

August 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Kocha Sebastien Migne amejitokeza kusema hana chuki na Kenya baada ya kandarasi yake ya miaka mitatu kukatizwa kighafla Agosti 12, 2019.

Migne, 46, alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Radio France Internationale (RFI).

Shoka liliwasili siku chache baada ya Kenya kulemewa na Tanzania ikitafuta tiketi ya kushiriki soka ya Afrika ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao (CHAN) mwaka 2020.

Harambee Stars ilitoka sare 0-0 jijini Dar es Salaam na kuandikisha matokeo sawia uwanjani Kasarani jijini Nairobi kabla ya kuzidiwa ujanja katika upigaji wa penalti za kuamua mshindi 4-1. Kandarasi ya Migne ilianza Mei 3 mwaka 2018 na ilitarajiwa kukatika Juni 30, 2021.

Pata mahojiano yote hapa chini:

RFI: Sebastien Migne, wewe si kocha tena wa timu ya taifa ya Kenya. Kitu gani kilichangia hali hii?

Sebastien Migne: Niliajiriwa na Kenya kujaribu kuona timu yake ya taifa inafuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) la mwaka 2019 ama 2021. Na kwa hivyo, nilitimiza jukumu hili mapema kuliko ilivyotarajiwa. Lengo limetimizika. Kwa hivyo, ulikuwa wakati mzuri kwangu, pengine, kutafuta changamoto mpya.

Na kisha, kuhusu Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), nilisukuma kila mtu kidogo ili tuweze kufuzu. Nadhani hatua niliyochukua itawafaa Wakenya kupata mwelekeo mpya.

Kwa ufupi, nadhani kuondoka kwangu kulifaa kila mtu ili tujitafutie maisha mapya.

RFI: Kwa hivyo, unaondoka (Kenya) bila chuki yoyote?

Sebastien Migne: La hasha! Ni nchi nzuri sana! Nimeishi humo miezi 16 nikifanya kazi na maafisa wengine wa benchi la kiufundi na pia wachezaji wangu. Familia yangu, ambayo ilinifuata Kenya, inafurahia nchi hii sana. Nikiwa bado sijapata kazi nyingine, nitaendelea kuishi humo.

Kwa hivyo, siondoki nikiwa na machungu. Nitatumai kipindi hicho kama funzo. Hata hivyo, kuna wakati (kocha) Zinedine Zidane, alifika mahali alitaka kuachana na Real Madrid. Sisi hatukuwa na la ziada, bali kuendelea na maisha yetu.

Nadhani kivyangu, kilikuwa kitu kizuri kwa kila mtu. Pia, ilinifaa kuondoka nikijua kuwa nilitimiza lengo langu licha ya changamoto ambazo hupatikana katika mataifa ya Afrika. Ni kitu kizuri kuondoka kutafuta maisha mapya.

Sasa, najirejesha sokoni. Wacha tusubiri tuone kitakachotokea katika wiki chache ama miezi ijayo.

RFI: Nini utakumbuka sana kama kitu kilichokufurahisha ukiwa kocha mkuu wa Harambee Stars?

Sebastien Migne: Kuna vitu kadhaa. Sitasahau ushindi dhidi ya Ghana katika mechi za kufuzu kushiriki Afcon.

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25 Kenya ilifanikiwa kuchapa timu ya Afrika inayoorodheshwa ndani ya mduara wa tano-bora kwenye viwango bora vya bara hili.

Pia, kuna mechi dhidi ya Ethiopia ambayo ilitufungulia milango ya kufuzu kushiriki Afcon 2019; uwanja ulikuwa umefurika. Nadhani ilikuwa mara ya kwanza kabisa uwanja (Kasarani) ulikuwa umefurika na mashabiki kiasi hicho wakati timu ya taifa ikicheza.

Ushindi wa mabao 3-0 nyumbani (dhidi ya Ethiopia) ni mojawapo ya kumbukumbu zangu kubwa.

Kwa bahati mbaya, fainali za Afcon hazikutuendea vyema. Tulijipata katika kundi ambalo hatimaye lilitoa timu mbili zilizofika fainali – Algeria na Senegal. Pia, tulisumbuliwa na majeraha.

Wakati wa mechi za kufuzu, hata hivyo, tulichukuliwa kama timu ngumu kucheza nayo, tukikamilisha mechi zetu nyingi bila kufungwa bao. Kwa hivyo, ilikuwa muhimu kujisuka siku za mwishomwisho kabla ya Afcon. Ilikuwa vigumu… Viwango vya Afcon vilituzidi. Ni aibu.

Baadaye, tuliwapa matumaini mashabiki wa Kenya. Na hilo lilikuwa jambo nzuri kwa sababu watu walikuwa wamesikitishwa na timu hii ya taifa.

Matumaini huongeza matarajio. Je, tunaweza kutimiza matarajio haya? Hilo ndilo swali nilijiuliza. Na sikuwa na uhakika. Kwa hivyo, kilikuwa kitu kizuri mimi kuenda zangu.