Michezo

Makiwa Kenya kumpoteza babake mwanariadha David Rudisha

March 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

RAIS Uhuru Kenya ameongoza Wakenya kuomboleza kifo cha jagina Daniel Rudisha, babake mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800.

“Natoa rambirambi zangu kwa familia na rafizki za Mzee Daniel Rudisha. Mzee Rudisha alikuwa shujaa wa riadha wa Kenya, mmoja wa wawakilishi wa kwanza wa Kenya katika Olimpiki, kocha na mwalimu ambaye alikuza vipaji vingi katika riadha. Kwa David Rudisha na familia yako yote, maombi yangu yako nanyi,” Rais Kenyatta ameandika katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter mnamo Alhamisi.

David Lekuta Rudisha alipoteza babake Daniel Matasi Rudisha siku ya Jumatano usiku ikiwa ni Machi 6, 2019.

Kulingana na David, mwendazake Daniel, ambaye alizaliwa Agosti 11 mwaka 1945, aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo baada ya kuwa hospitalini kwa siku kadhaa.

Daniel alikuwa mkimbiaji wa mbio fupi hasa za mita 400. Alizaliwa katika eneobunge la Kilgoris katika kaunti ya Kajiado.

Alipeperusha bendera ya Kenya katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1968 mjini Mexico City nchini Mexico katka mbio za kupokezana vijiti za mita 4×400 akishinda medali ya fedha akishirikiana na Munyoro Nyamau, Naftali Bon na Charles Asati.

Daniel pia alitimka katika mbio za mita 400 katika makala hayo ya Olimpiki akiondolewa katika robo-fainali. Baada ya kustaafu kukimbia, Daniel aliajiriwa kama mwalimu na pia kocha. Kama kocha, amenoa wakimbiaji wengi watajika wakiwemo ndugu Billy Konchellah, ambaye alishinda mbio za mita 800 katika Riadha za Dunia mwaka 1987 mjini Roma nchini Italia.

David, 30, anashikilia rekodi ya mbio za mita 800 ya dakika 1:40.91 aliyoweka katika michezo ya Olimpiki jijini London, Uingereza mwaka 2012.

Kifo cha Daniel Rudisha kimewasili baada ya Kenya kupoteza jagina mwingine Nyantika Mayoro mnamo Februari 24 na Naftali Bon mnamo Novemba 2, 2018. Makiwa!