Makocha wengi wang'ang'ania nafasi ya kunoa #KenyaSevens
Na Geoffrey Anene
SHUGHULI ya kuomba kazi ya kocha mkuu wa timu ya Kenya Sevens imefungwa Septemba 7, 2018, huku Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) likifichua limepokea maombi kutoka Kenya, Afrika Kusini na Bara Ulaya.
Mkurugenzi wa Raga wa KRU, Thomas Odundo amesema KRU itajua idadi kamili ya maombi Septemba 8 na kuyapitia na kisha kutangaza majina ya walioomba kazi hapo Septemba 10.
“Tutaandaa mahojiano na kila mmoja wao na kisha kufanya mazungumzo kuhusu mshahara wanaotarajia kupata. KRU inapitia wakati mgumu wa kifedha wakati huu kwa hivyo hatutafuti kocha ambaye ataitisha mshahara mkubwa sana ambao hatutaweza kumudu.
Tumepata maombi kutoka Kenya, Afrika Kusini, Zimbabwe na Bara Ulaya. Hakuna mtu kutoka nje ya maeneo haya ameomba kazi, lakini bado kuna muda kwa sababu makataa ya kufanya hivyo ni saa sita usiku Ijumaa (Septemba 7),” Odundo amesema.
Ingawa kocha wa sasa wa Shujaa, Innocent Simiyu, alisema Agosti 30 halengi kuomba kunoa timu hii tena kandarasi yake itakapotamatika mwisho wa mwezi ujao wa Oktoba, Odundo amesema yuko huru kuomba kazi hiyo.
“Hatujui kama Simiyu ameomba kuendelea kuongoza Shujaa. Tunavyozungumza wakati huu, bado ana kandarasi na timu hii na chochote chawezekana,” ameongeza.
Kocha wa zamani wa Kenya, Mike Friday alionekana kumshauri Simiyu kuendelea kuongoza Shujaa alipochapisha ujumbe wa kumsifu kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter saa chache baada ya KRU kuomba makocha waombe kazi ya kocha mkuu.
“Wewe ni kocha mzuri na mtu mzuri na tunaona mambo yanaendea Shujaa vizuri katika Raga ya Dunia. Natumai suluhu itapatikana na utaweza kuendelea na kazi hiyo nzuri wewe na vijana wako mnafanya.”
Simiyu, ambaye aliongoza Shujaa kuvuna alama za kihistoria (104) msimu 2017-2018, alijibu Mungereza huyo, “…Tulitumiwa notisi huduma zetu hazitahitajika kwa sababu KRU inapitia hali ngumu ya kifedha.”