Michezo

MALI YA JUVE: Matthijs de Ligt atua mjini Turin

July 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA na CHRIS ADUNGO

NAHODHA na beki matata wa Ajax Amsterdam na timu ya taifa ya Uholanzi, Matthijs De Ligt, 19, ametua mjini Turin, Italia kuufanya rasmi uhamisho wake hadi kambini mwa Juventus kwa kiasi cha Sh8.8 bilioni.

Hadi alipohiari kujiunga na Juventus ambao ni miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), De Ligt alikuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona, Paris Saint-Germain (PSG) au Manchester United.

De Ligt aliachwa nje ya kikosi cha Ajax kilichoelekea nchini Austria wikendi iliyopita kujifua kwa minajili ya kampeni za msimu mpya.

Chini ya unahodha wake, Ajax walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uholanzi (Eridivisie) na Dutch Cup.

Pia walitinga hatua ya nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita baada ya kuwabandua Juventus na waliokuwa mabingwa watetezi wa kipute hicho, Real Madrid. Pia alikuwa katika kikosi cha timu ya Uholanzi kilichotinga fainali ya Nations League japo walipepetwa na Ureno 1-0 na Ureno mwezi jana.

De Ligt aliingia katika sajili rasmi ya Ajax akiwa kitoto cha umri wa miaka tisa pekee na kufikia sasa, anajivunia rekodi ya kuwafungia waajiri wake hao mabao 13 kutokana na jumla ya michuano 117.

Nahodha

Aliwajibishwa na Ajax kwa mara ya kwanza mnamo 2016 na akapokezwa utepe wa unahodha mnamo Machi 2018.

Chipukizi huyu alivalia jezi ya timu ya taifa ya Uholanzi kwa mara ya kwanza mnamo Machi 2017 hata ingawa wakati huo alikuwa amewajibishwa na Ajax mara mbili pekee katika michuano ya Ligi Kuu.

PSG ambao wamejivunia ukiritimba wa Ligi wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kwa kipindi kirefu, walikuwa radhi kumpokeza De Ligt mshahara wa hadi Sh51 milioni kwa wiki iwapo angekubali kujiunga nao.

Japo ameingia katika sajili rasmi ya Juventus, Mino Raiola ambaye ni wakala wa De Ligt, amekiri kwamba yalikuwa matamanio ya mteja wake huyo kutua kambini mwa Barcelona nchini Uhispania.