Michezo

Malkia Strikers kufufua uhasama dhidi ya Cameroon fainali ya voliboli

July 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na Cameroon zitakutana katika fainali ya mashindano ya voliboli ya wanawake ya Bara Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya kujikatia tiketi jijini Cairo nchini Misri mnamo Jumamosi usiku.

Saa chache baada ya Malkia Strikers ya kocha Shaileen Ramdoo kubwaga Senegal kwa seti 3-0 (25-13, 25-13, 25-20) katika nusu-fainali ya kwanza, mabingwa watetezi Cameroon waliandikisha ushindi sawa na huo dhidi ya washindi wa zamani Misri 3-0 (25-23, 25-21, 25-18).

Kenya ilichapwa na Cameroon 3-0 (25-22, 25-19, 29-27) katika fainali ya makala yaliyopita ambayo yalifanyika mjini Yaounde mwaka 2017.

Timu hizi mbili tayari zimekutana katika mashindano haya. Kenya ilitolewa kijasho chembamba kabla ya kulemea Cameroon 3-2 (18-25, 16-25, 27-25, 30-28, 15-10) katika mechi ya mwisho ya Kundi B mnamo Julai 11.

Tangu mwaka 2003, Kenya na Cameroon zimekutana katika mashindano haya mara saba. Kabla ya kuchapwa 3-0 mwaka 2017, Kenya ilikuwa imechabanga Cameroon 3-0 katika nusu-fainali mwaka 2003, 3-0 katika mechi za makundi (2007), 3-0 katika mechi za makundi (2011), 3-0 katika mashindano ya mzunguko (2013) na 3-0 katika nusu-fainali (2015).

Cameroon imeonyesha imeimarika kwa hivyo haitakuwa kazi rahisi kwa Kenya katika fainali.

Ratiba ya siku ya mwisho (Julai 14):

Saa kumi na moja jioni – Morocco na Algeria (Mechi ya kuamua nambari tano na sita);

Saa moja usiku – Misri na Senegal (mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba);

Saa tatu usiku – Kenya na Cameroon (fainali)