• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Malkia Strikers matumaini tele watabwaga Ethiopia

Malkia Strikers matumaini tele watabwaga Ethiopia

Na GEOFFREY ANENE

KENYA inaamini iko katika nafasi nzuri ya kufukuzia ushindi wake wa pili mfululizo kwenye mchujo wa voliboli ya wanawake ya Ukanda wa Tano ya All-African Games itakapomenyana na Ethiopia jijini Kampala, Uganda, Jumatatu jioni (6.00pm).

Kocha Josp Barasa, ambaye ni mmoja wa makocha wa Malkia Strikers walio nchini Uganda kwa kipute hiki, ameambia Taifa Leo kwamba, “Tuliona Ethiopia ikicheza dhidi ya Uganda na ni timu tunaweza kudhibiti kupitia kwa kuanzisha mipira vizuri, kuzuia makombora yao na kuwa na ulinzi imara. Walipoteza dhidi ya Uganda nasi tukapiga Rwanda, kwa hivyo tuko katika nafasi nzuri kuwaliko.”

Motisha ya Kenya inatokana na kuanza kampeni yake ya kufika katika ulingo wa Bara Afrika kwa kupepeta Rwanda kwa seti 3-0 (25-10, 25-17, 25-10) mnamo Mei 19.

Kuhusu mechi ya mwisho dhidi ya Uganda hapo Mei 21, Barasa ametahadharisha Malkia Strikers dhidi ya kuona wenyeji hawa kama wanyonge watakapokutana jijini Kampala, Jumanne.

Katika mahojiano Jumatatu, Barasa amesema, “Tulishuhudia wakicheza dhidi ya Ethiopia na ukweli ni kwamba Waganda wameimarika sana. Pia, wako nyumbani na ninaamini itakuwa mechi ngumu. Hatuwafahamu vyema sana kwa sababu hatujakutana nao kwa muda mrefu.”

Barasa ni mmoja wa makocha wa Malkia Strikers inayowania tiketi moja ya kufika mashindano ya All-African Games katika mechi za Ukanda wa Tano jijini Kampala.

Uganda, ambayo iliratibiwa kukabiliana na Rwanda hapo Jumatatu, ililima Ethiopia 3-0 (25-17, 25-19, 25-13).

Mshindi wa mchujo huu unaoleta pamoja mataifa manne ataingia All-African Games itakayofanyika nchini Morocco mwezi Agosti mwaka huu.

Kenya ni mabingwa watetezi wa All-African Games baada ya kuchapa Cameroon 3-1 katika fainali jijini Brazzaville, Congo mwaka 2015.

You can share this post!

Jumwa ashangaza kusema Ruto ndiye ‘Mungu’

Kenya yaanza Kriketi ya Afrika kwa kuliza Nigeria

adminleo