Malkia Strikers wailima Ethiopia kunusia All African Games
Na GEOFFREY ANENE
MALKIA Strikers iko pua na mdomo kuingia mashindano ya All-African Games baada ya kubwaga Ethiopia kwa seti 3-0 kwenye mchujo wa Ukanda wa Tano wa voliboli ya wanawake jijini Kampala nchini Uganda, Jumatatu.
Mabingwa wa All-African Games mwaka 1991, 1995, 1999 na 2015 Kenya walienda katika mapumziko ya kwanza mawili ya lazima wakiongoza seti ya kwanza kwa alama 8-3 na 16-8 kabla ya kuinyakua 25-13.
Kenya ilikuwa katili zaidi katika seti ya pili ambayo iliongoza 11-2, 16-5 na 20-6 kabla ya kuishinda 25-8.
Malkia, ambayo inanolewa na makocha Shailene Shamdoo (Italia), Japheth Munala na Josp Barasa, ilikamilisha kazi kwa kubeba seti ya tatu kwa alama 25-10 baada ya kuongoza 9-3 na 17-8.
Wakenya wako juu ya jedwali la mchujo huu wa mataifa manne kwa alama sita. Waliingia mechi ya Ethiopia na motisha ya kucharaza Rwanda 3-0 (25-10, 25-17, 25-10) mnamo Mei 19.
Ethiopia imebanduliwa nje ya kampeni ya kufika All-African Games nchini Morocco mwezi Agosti mwaka 2019.
Waethiopia waliteremka katika ukumbi wa Lugogo kumenyana na Kenya wakiwa wanauguza kichapo cha seti 3-0 dhidi ya Uganda. Kenya na Uganda zitakabiliana Mei 21. Uganda itamenyana na Rwanda katika mechi yake ya pili baadaye Mei 20.
Kikosi cha Kenya: Mercy Moim, Sharon Chepchumba, Noel Murambi, Leonida Kasaya, Violet Makuto, Immaculate Chemutai, Jane Wacu, Janet Wanja, Edith Wisa, Triza Atuka, Lorine Chebet na Agripina Kundu.