Michezo

Malkia Strikers yafunzwa voliboli Italia

August 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imejifunza mengi kutokana na vichapo vitatu vikali ilivyopokea dhidi ya Italia, Uholanzi na Ubelgiji kwenye mashindano ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 yaliyofanyika mjini Catania kutoka Agosti 2-4, 2019.

Malkia Strikers ililimwa kwa seti 3-0 dhidi ya Italia za alama 25-17, 25-10 na 25-14, ikazabwa 3-0 (25-17, 25-10, 25-10) dhidi ya Uholanzi na kupepetwa 3-0 (25-15, 25-14, 25-7) dhidi ya Ubelgiji.

Italia ilifuzu kushiriki Olimpiki baada ya kushinda mechi zake zote tatu bila kupoteza seti hata moja. Uholanzi ilikamilisha ya pili, Ubelgiji ya tatu nayo Kenya ikavuta mkia.

Baada ya mashindano haya kukamilika, Taifa Leo ilizungumza na mmoja wa makocha wasaidizi wa Kocha Mkuu Shaileen Ramdoo, Josp Barasa.

“Tumepata mafunzo mengi kutoka mashindano haya. Kwanza kabisa ni jinsi ya kuanzisha mipira. “Service” ni muhimu sana. Tunahitaji kuwa na “service” nzuri. Tukifaulu kuwa na “service” za kuruka juu na zenye kasi ya juu zitatusaidia sana kuinua mchezo wetu.

“Pili, tunafaa kupunguza makosa yetu katika idara zote – ujuzi, “service”, kupakua mipira (setting), kufanya mashambulizi, ulinzi na mbinu za kuzuia makombora. Tatu, hatuna budi kuwekeza katika wachezaji warefu. Tumeona hapa kuwa urefu una manufaa yake.

“Nne na mwisho, tunahitaji kuwa na benchi la kiufundi la zaidi ya makocha watano, ambao kila mmoja anashughulikia majukumu tofauti. Tukizingatia haya, naamini tutaimarisha mchezo wetu na kupiga hatua kimataifa,” amesema kocha huyo mkuu wa klabu ya Kenya Prisons katika mahojiano kutoka nchini Italia.

Kenya imewahi kushiriki voliboli ya wanawake kwenye Olimpiki mara mbili – mwaka 2000 mjini Sydney nchini Australia, ambayo pia ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa, na mwaka 2004 mjini Athens nchini Ugiriki.

Ilikosa makala ya mwaka 2008 mjini Beijing nchini Uchina, mwaka 2012 mjini London nchini Uingereza na mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.

Itakuwa na kibarua kigumu kufuzu kushiriki makala yajayo yatakayofanyika mjini Tokyo nchini Japan kwa sababu kufikia sasa hakuna timu kutoka Afrika imefuzu.

Inamaanisha kuwa italimana na wakali wa Cameroon, Misri, Algeria, Senegal na Tunisia, miongoni mwaka timu zingine, Januari mwaka 2020 kutafuta tiketi moja ilioko mezani.