Malkia Strikers yatinga fainali voliboli ya wanawake ya Bara Afrika
Na GEOFFREY ANENE
KENYA imeingia fainali ya mashindano ya voliboli ya wanawake ya Bara Afrika baada ya kulipua Senegal katika nusu-fainali kwa seti 3-0 (25-13, 25-13, 25-20) iliyochezwa Jumamosi jijini Cairo nchini Misri.
Malkia Strikers ya kocha Shaileen Ramdoo inatafuta kuimarisha rekodi yake hadi mataji 10. Itakabiliana na Misri/Cameroon katika fainali Jumapili.
Mnamo Alhamisi usiku, Kenya ilitoka chini seti mbili na kuzima mabingwa watetezi Cameroon kwa seti 3-2 katika mechi ya mwisho ya Kundi B.
Malkia Strikers, ilikodolea macho kupoteza mechi ya pili mfululizo mikononi mwa Cameroon ilipoonyeshwa kivumbi katika seti mbili za kwanza 25-18 na 25-16, mtawalia.
Hata hivyo, Kenya, ambayo ililimwa na Cameroon seti 3-0 katika fainali ya makala yaliyopita jijini Yaounde mwaka 2017, ilijikakamua na kushinda seti ya tatu 27-25 na kisha ikasawazisha seti 2-2 ilipobeba seti ya nne 30-28 kabla ya kukamilisha kazi kwa kunyakua seti ya tano 15-10.
Ushindi huu wa Kenya wa sita katika mechi saba dhidi ya Cameroon kwenye kombe hili tangu mwaka 2003, uliwezesha Malkia Strikers kumaliza juu ya kundi lake na hivyo kukwepa kukutana na wenyeji Misri katika nusu-fainali.
Senegal ilimaliza ya pili katika Kundi A baada ya kupepeta Morocco 3-0 (27-25, 25-11, 25-17).
Washindi wa Kundi A Misri watamenyana na nambari mbili kutoka Kundi B Cameroon baadaye Jumamosi usiku katika nusu-fainali ya pili.
Ijumaa ilikuwa siku ya mapumziko kabla ya mechi za nusu-fainali hapo Jumamosi.
Mara ya mwisho Kenya ilikutana na Senegal ilikuwa katika mechi za makundi mwaka 2017.
Malkia Strikers iling’ara 3-0. Kenya pia ilipatia Senegal dozi sawa na hiyo mwaka 2013 na 2011.
Fainali ni , Jumapili, Julai 14, 2019.
Kikosi cha Kenya:
Wachezaji – Jane Wacu, Janet Wanja, Brackcides Khadambi, Edith Mukuvilani Wisa, Trizah Atuka, Gladys Ekaru, Violet Makuto,
Emmaculate Chemtai, Mercy Moim (nahodha), Noel Murambi, Sharon Chepchumba, Leonida Kasaya, Elizabeth Wanyama na Agripina Kundu.
Benchi la kiufundi – Ramdoo Shailen (Kocha Mkuu), Japheth Munala (Naibu wa kocha wa kwanza), Josp Barasa (Naibu wa kocha wa pili), Charles Maina (Daktari wa mazoezi ya viungo), David Lung’aho (Mkurugenzi wa kiufundi/Meneja wa timu).