Malkia Strikers yatumia wembe ulionyoa Rwanda na Ethiopia kukata Uganda na kuingia All-African Games
Na GEOFFREY ANENE
KENYA ilitolewa kijasho na Uganda katika seti ya kwanza kabla ya kuwanyoa seti 3-0 katika mechi ya mwisho ya Ukanda wa Tano na kufuzu kushiriki voliboli ya wanawake kwenye mashindano ya Bara Afrika (All-African Games) Jumanne katika ukumbi wa Lugogo jijini Kampala.
Malkia Strikers ilikuwa alama moja tu mbele ya Uganda 21-20 katika seti ya kwanza kabla ya kushinda wenyeji hao 25-20.
Baada ya kubabaishwa katika seti ya kwanza, Kenya ilirejea katika seti mbili zilizofuata kwa nguvu zaidi na kuzinyakua 25-17, 25-16, mtawalia.
Majirani hawa waliingia fainali wakiwa wamechapa Rwanda na Ethiopia.
Kenya ilikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufuzu kutetea ubingwa wake wa Afrika kwa sababu haikuwa imepoteza seti ikilinganishwa na Uganda iliyohitaji ushindi dhidi ya Wakenya kutokana na kuwa ilikuwa imekubali Rwanda kushinda seti moja.
‘Uganda mlima’
Baada ya mechi hii ambayo Jane Wacu, Mercy Moim, Edith Wisa, Triza Atuka, Noel Murambi, Violet Makuto na Agrippina Kundu walianzishwa, kambi ya Kenya iliyojawa na furaha ilikiri kwamba Uganda haikuwa timu rahisi.
“Kazi nzuri kutoka kwa kila mchezaji wetu. Tulitarajiwa kama mabingwa wa Afrika kuwa na presha. Hata kama tumeibuka na ushindi, bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili tuwe imara,” Mwitaliano Shailene Shamdoo alisema.