• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
MALKIA WA CECAFA: Harambee Starlets yazima Kilimanjaro Queens

MALKIA WA CECAFA: Harambee Starlets yazima Kilimanjaro Queens

Na GEOFFREY ANENE

JENTRIX Shikangwa alikuwa shujaa wa Kenya alipofungia Harambee Starlets mabao yote yaliyoiwezesha kunyakua ubingwa wa soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kuzima Kilimanjaro Queens ya Tanzania 2-0 katika fainali iliyogaragazwa Jumatatu jijini Dar es Salaam.

Warembo wa kocha David Ouma walisubiri hadi dakika 20 za mwisho kupata magoli hayo yaliyowawezesha kuandikisha historia ya kuwa taifa la pili kubeba taji hili baada ya Tanzania mwaka 2016 na 2018 na Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Tanzania, mwaka 1986.

Shikangwa, 17, alifungua ukurasa wa magoli kupitia kwa penalti safi. Alimwaga kipa Najat Abass baada ya Donisia Minja kunawa mpira ndani ya kisanduku chake cha Tanzania.

Kenya ilikuwa imepata nafasi yake nzuri ya kwanza katika dakika ya 24, lakini kipa Najat Abass akapangua frikiki ya Mwanahalima Adam kwa urahisi.

Baada ya saa nzima bila bao, Shikangwa, ambaye aliingizwa uwanjani kama mchezaji wa akiba, hakusikitisha ila upesi alisaidia Kenya kuvuna taji hilo lake la kwanza kabisa.

Aliona lango kupitia penalti dakika ya 70 kabla ya kuzamisha kabisa chombo cha Tanzania dakika ya 87 kupitia kwa shuti moto.

Shikangwa amefunga katika mechi zote tanona kuwezesha Starlets kukamilisha kampeni yake bila kupoteza. Aliibuka mfungaji bora kwa mabao 10.

Kabla ya Kenya kutwaa taji hili bila nyavu zake kuchanwa hata mara moja, Tanzania ilikuwa imetawala makala mawili mfululizo ikiwemo kuchabanga Kenya 2-1 katika fainali ya mwaka 2016 pamoja na Zanzibar kutawala mwaka 1986.

Uganda yaridhika na shaba

Mwaka 2019 Crested Cranes ya Uganda iliridhika na medali ya shaba baada ya kubwaga Burundi 2-0 katika mechi ya kutafuta nambari tatu.

Amina Nababi na Shamira Nalujja walifungia washindi wa nishani ya fedha mwaka 2018 Uganda mabao hayo muhimu dakika 62 na 82, mtawalia.

Burundi ilikuwa inarejea katika mashindano haya baada ya kukosa makala ya mwaka jana yaliyofanyika nchini Rwanda.

Ilichapwa na Uganda 1-0 katika mechi za makundi za mwaka 2016 nchini Uganda wakati Kenya na Tanzania zilipofika fainali.

Timu nyingine zilizoshiriki mashindano haya mwaka huu, lakini zikaondolewa katika mechi za makundi ni Ethiopia na Sudan Kusini, ambazo zilishinda mechi moja, nazo Zanzibar na Djibouti zikaambulia pakavu.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nina virusi ilhali yeye hana, naogopa...

Real Madrid waalika PSG kwa mtihani mkali wa Uefa

adminleo