Man City, Arsenal ni kufa kupona UEFA
BAADA ya mkondo wa kwanza kumalizika kwa sare ya 3-3 katika uwanja wa Santiago Bernabeu nchini Uhispania, leo usiku Manchester City watakuwa nyumbani ugani Etihad kualika Real Madrid katika robo-fainali ya ya marudiano ya Klabu Bingwa (UEFA).
Katika pambano jingine linalotarajiwa kuvutia mashabiki wengi ugani Alianz Arena jijini Munich, wenyeji Bayern Munich watakaribisha Arsenal baada ya timu hizo kutoka sare ya 2-2 katika mkondo wa kwanza ugani Emirates.
Vijana wa Mikel Arteta wanaingia uwanjani baada ya mwishoni mwa wiki kupigwa 2-0 na Aston Villa katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kichapo ambacho kimepunguza matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Bayern Munich wamekuwa wakisuasua kwenye mechi za ligi ya nyumbani – Bundesliga, hali inayomfanya Arteta asiwe na wasiwasi kuhusu ziara ya kikosi chake nchini Ujerumani.
Bayern wanajivunia rekodi nzuri dhidi ya Arsenal, ya ushindi mara saba katika mechi 13, Arsenal wakiwa na ushindi mara tatu pekee.
Itakuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kufuzu kwa nusu-fainali ya UEFA tangu msimu wa 2008-09. Wamepoteza mechi tatu ugenini dhidi ya timu za Ujerumani, wakipokea kichapo cha 5-1 dhidi ya Bayern Munich katika mechi ya mwisho.
Arsenal walicheza vizuri katika mkondo wa kwanza, lakini wana rekodi mbaya ugani Allianz Arena.
Ugani Etihad, kocha Pep Guardiola anatarajiwa kupanga kikosi imara baada ya kurekebisha makosa yaliyovuruga matumaini ya kufunga mabao ya kutosha ugenini, licha ya kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa.
Kulingana na wadadisi wa soka, Madrid watazua upinzani mkali katika pambano hili, lakini wenyeji wanatarajiwa kuwa katika hali njema kutokana na kuimarika kwa viwango vya kiungo Kevin De Bruyne na mshambuliaji matata Erling Haaland.
Huenda Guardiola akapanga kikosi chake bila Nathan Ake, John Stones, kipa Ederson na Kyle Walker wanaouguza majeraha, lakini raia huyo wa Uhispania anajivunia rekodi nzuri ya mechi za nyumbani tangu achukue usukani.
Kwa upande mwingine, kocha Carlo Ancelotti atapanga timu yake bila David Alaba na Thibaut Courtois wakati wa ziara hii ambayo inatarajiwa kuwa na changamoto kwa kikosi chake ambacho kimekuwa na safu imara ya ulinzi msimu huu.
Madrid wataingia uwanjani kujaribu kuzuia yaliyotokea msimu uliopita ambapo baada ya sare ya 1-1 ugani Bernabeu katika hatua ya nusu-fainali, walibanduliwa kutokana na kichapo cha 4-0 ugani Etihad.
Vinicius Junior na De Bruyne walifunga katika mkondo wa kwanza, lakini mabao mawili ya Bernardo Silva na mengine ya Manuel Akanji na Julian Alvarez yaliangamiza matumaini ya Madrid.
Katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ugani Bernabeu, Bernardo Silva alitangulia kufunga bao la mapema baada ya Jack Grealish kufanyiwa madhambi na Aurelien Tchoumameni karibu na eneo la hatari.
Madrid walisawazisha kupitia kwa Ruben Dias dakika 10 baadaye, kabla ya kuongeza bao la pili kupitia kwa Rodrygo.
City walijipatia bao la pili kupitia kwa Phil Foden, huku Jasko Gvardiol akifunga bao la tatu kabla ya Federico Valverde kusawazisha kufuatia kombora kali kutoka upande wa kulia.
Katika mechi zao tano zilizopita, Manchester City wameshinda mara tatu na kutoka sare mara mbili, mechi ya mwisho dhidi ya Luton ikimalizika kwa ushindi mkubwa wa 5-1.
Real Madrid kwa upande wake, wamekuwa katika kiwango kizuri huku wakijivunia ushindi mara nne katika mechi tano zilizopita, ukiwemo ushindi wa 4-0 dhidi ya Celta Vigo katika mechi ya mwisho kwenye Ligi Kuu ya Uhispania – La Liga.