Michezo

Man City, Barcelona, Liverpool au Juventus pazuri kunyakua UEFA

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CHRIS ADUNGO

UPO uwezekano mkubwa kwa mshindi wa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula huu kutokea nchini Uingereza. Klabu hiyo ni ama Man-City au Liverpool. Si ajabu iwapo wawili hawa watakutana katika fainali.

Chelsea iliyopiga Bayern Munich 4-3 kupitia penalti mnamo 2011-12, ndiyo klabu ya mwisho inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuwahi kutia kapuni ufalme wa UEFA.

Droo ya robo-fainali ya UEFA itakayowakutanisha Manchester City na Tottenham Hotspur, Liverpool na FC Porto, kisha Manchester United na Barcelona msimu huu ni afueni kubwa kwa timu za EPL.

Mshindi kati ya Tottenham na Man-City atamenyana na atakayetamalaki mechi kati ya Ajax na Juventus katika nusu-fainali. Aidha, mshindi kati ya Barcelona na Man-United atavaana ama na Liverpool na au Porto katika nusu-fainali nyingine.

Historia inawaweka Barcelona katika nafasi nzuri zaidi ya kuwapepeta Man-United na kutinga nusu-fainali ambayo kwa asilimia kubwa, huenda iwakutanishe na Liverpool?

Man-United wanajivunia kushinda Barcelona mara moja pekee katika jumla ya mechi nane zilizopita. Vijana hawa wa kocha Ole Gunnar Solskjaer wataanza kampeni yao dhidi ya Barcelona ugani Old Trafford ili wasicheze mchuano wa mkondo wa pili kwa wakati mmoja na majirani zao wa jiji la Manchester.

Man-United walitawazwa mabingwa wa UEFA mara ya mwisho mnamo 2008 baada ya kuwalaza Chelsea nchini Urusi. Mwaka huo, waliwabandua Barcelona ambao ni mabingwa mara tano wa UEFA katika hatua ya nusu-fainali.

Man-City ambao wanafukuzia jumla ya mataji manne msimu huu wanapigiwa upatu wa kuendeleza ubabe wao dhidi ya Tottenham.

Mabingwa hawa watetezi wa taji la EPL tayari wanajivunia rekodi nzuri ambayo imewashuhudia wakiwachabanga Tottenham katika jumla ya mechi tatu zilizopita. Miamba hawa wawili wa EPL wanatafuta taji lao la kwanza la UEFA muhula huu.

Ushindi kwa Man-City utawapa hamasa zaidi ya kuwapepeta Juventus katika nusu-fainali. Juventus wanaojivunia huduma za Cristiano Ronaldo, wanatazamiwa kuwazima Ajax mapema katika robo-fainali.

Ajax ambao ni wafalme mara nne wa UEFA, hawana ushindi katika mechi tatu dhidi ya mabingwa wa zilizopita dhidi ya Juventus waliotawazwa mabingwa mnamo 1985 na 1996.

Liverpool ambao pia ni mabingwa mara tano wa UEFA, hawajapoteza dhidi ya Porto katika jumla ya mechi sita zilizopita. Makali ya Liverpool ambao pia wanatarajiwa kuwapiga kumbo Man-City kileleni mwa jedwali la EPL, yatawapa wakati mwepesi katika robo-fainali.

Hili la kushinda Porto likitimia, basi mtihani mgumu zaidi uliopo mbele ya Liverpool ni kuwapepeta Barcelona ambao iwapo wataponea, basi watajiweka pazuri kunyanyua ubingwa wa UEFA msimu huu kwa kuwapiku ama Man-City au Juventus.