Man City mawindoni kutia presha vinara Arsenal, Liverpool kileleni
MANCHESTER, UINGEREZA
NAMBARI tatu Manchester City leo wataalika Luton Town (18) ugani Etihad katika mechi ambayo hawana budi kushinda ili kudumisha presha dhidi ya viongozi Arsenal na nambari mbili Liverpool katika vita vya farasi watatu kwenye Ligi Kuu.
Man-City wanaotetea taji, wamejaa motisha baada ya kulipua Crystal Palace 4-2.
Vijana wa kocha Pep Guardiola, ambao pia jicho moja liko kwa mechi ya robo-fainali ya marudiano ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, hawajapoteza ugani Etihad msimu huu.
City wanaofukuzia taji la nne mfululizo ligini, wataanza mchuano huo na asilimia kubwa ya kuushinda, hasa kwa sababu pia wana rekodi nzuri dhidi ya Luton ya ushindi mara 22, sare 15 na kupoteza 14.
Hawajapoteza 10 mfululizo dhidi ya Luton katika mashindano yote.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana ni Desemba 27 mwaka jana wakati City walitawala 6-2 kupitia mabao ya Erling Haaland (matano) na Mateo Kovacic.
Jordan Clark alifungia Luton siku hiyo. Luton watajitoa katika mduara hatari wa kutemwa wakifanya miujiza ya kupepeta City.
Macho pia yatakuwa kambini mwa nambari sita Manchester United wanaozuru Bournemouth (12).
Man-United ya kocha Erik ten Hag ililishwa kichapo cha 3-0 katika safari yake ya mwisho mjini Bournemouth mwezi Desemba 2023.
Soma pia: Kwa mara ya kwanza, uwezo wa Arsenal kutwaa ubingwa wa ligi umepita wa Liverpool – Ubashiri