Manchester City kumsajili Messi msimu ujao wa 2021-22
Na MASHIRIKA
MANCHESTER City wamefichua mpango wa kumsajili nyota Lionel Messi muhula ujao iwapo ataazimia kukatiza uhusiano wake na Barcelona na kuondoka ugani Camp Nou.
Messi aliduwaza mashabiki, wachezaji wenzake na wasimamizi wa Barcelona mnamo Agosti 2020 alipowaomba waajiri wake wamwachilie atafute hifadhi kwingineko.
Maamuzi hayo ya Messi, 33, yaliamsha hamu ya Manchester City, Juventus na Paris Saint-Germain (PSG) kutaka kumsajili Messi ambaye ni miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa.
Msukosuko ulioibuliwa na hatua hiyo ya Messi mwishowe ulitulizwa baada ya majuma mawili ya kushauriana kwingi.
Japo Messi alihiari kusalia ugani Camp Nou chini ya mkufunzi mpya Ronald Koeman, dalili zote zinaashiria kwamba sogora huyo hafurahii maisha yake kambini mwa Barcelona na ataikamia fursa yoyote ya kuondoka.
Kati ya vizingiti vilivyozuia uhamisho wa Messi hadi Man-City mwishoni mwa msimu wa 2019-20 ni maamuzi ya La Liga ambao walisisitiza kwamba mnunuzi wa Messi angelazimika kuweka mezani kima cha Sh89 bilioni ndipo amtwae kabisa kwa mujibu wa kifungu kwenye mkataba wake.
Afisa Mwendesha Shughuli kambini mwa Man-City, Omar Berrada, amesema kwamba watakuwa katika nafasi bora zaidi ya kumsajili Messi kuanzia Januari 2021 au baada ya mkataba wake kambini mwa Barcelona kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.
“Ni mwanasoka wa haiba kubwa ambaye ataleta mabadiliko makubwa katika soka ya Uingereza. Kwa sasa ndiye mchezaji bora zaidi duniani na ujio wake utabadilisha mtazamo wa wachezaji wengi wa EPL kuhusu soka,” akasema Berrada katika mahojiano yake na gazeti la M.E.N Sport.
Wakati uo huo, Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu anatazamiwa kuondoka mamlakani baada ya kampeni ya kupigwa kwa kura ya kutokuwa na imani naye kupata uungwaji mkono miongoni mwa wadau wa kikosi hicho cha La Liga.
Bartomeu alichaguliwa kuwa Rais wa Barcelona mnamo 2014 na uongozi wake umekashifiwa pakubwa kiasi cha kuhusishwa na maamuzi ya hivi karibuni ya Messi kutaka kuondoka ugani Camp Nou.
Mpango wa kuondolewa kwa Bartomeu kupitia kura ya maoni ulifichuliwa na vinara wa Barcelona siku moja baada ya Messi kuwasilisha barua ya kutaka kuachiliwa kuondoka Camp Nou.
Kufikia sasa, saini 20,731 kutoka kwa mashabiki na wasimamizi wa Barcelona wanaounga mkono mpango huo zimepatikana, kumaanisha kwamba Bartomeu yuko pua na mdomo kuondolewa mamlakani kupitia kura ya wadau kutokuwa na imani naye.
Ili kufanikisha maandalizi ya kura hiyo, jumla ya saini 16,500 pekee ndizo zilizohitajika kuwasilishwa na kukaguliwa na wahusika kabla ya Bartomeu, 57, kuondolewa kupitia refarenda chini ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Refarenda ya kumng’atua Bartomeu itashuhudia wanachama 150,000 wa Barcelona wakipiga kura na iwapo asilimia 66.5 ya wanachama watapiga kura ya kumwondoa, basi uongozi wake utafikia kikomo.
Bartomeu alitarajiwa kukamilisha rasmi kipindi chake cha uongozi cha mihula miwili mnamo Machi 2021.
Iwapo kura ya kutokuwa na imani naye itaandaliwa, basi atakuwa rais wa tatu wa Barcelona kuondolewa mamlakani kwa jaribio la njia hiyo baada ya Josep Lluis Nunez mnamo 1998 na Joan Laporta mnamo 2008. Mpango wa kung’atuliwa kwa wawili hao kupitia refarenda miaka hiyo haukufaulu.
Chini ya urais wa Bartomeu, Barcelona wamekabiliwa na visa vya matumizi mabaya ya fedha na kikosi hicho kilikamilisha kampeni za msimu huu bila kutwaa taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2008.
Walibanduliwa mapema na Athletic Bilbao kwenye Copa del Rey, wakapigwa kumbo na Real Madrid kwenye La Liga na kudhalilishwa na Bayern Munich kwa kichapo cha 8-2 kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).