Manchester City nje ya Uefa licha ya kulaza Spurs
MATUMAINI ya Manchester City kutwaa mataji manne msimu huu yaliyeyuka baada ya kubanduliwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA), Jumatatu usiku.
Vinara hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) waliondolewa na Tottenham Hotspur kwenye robo-fainali licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 katika mechi ya marudiano ugani Etihad, Uingereza.
Spurs ambao walipata ushindi wa bao 1-0 katika pambano la mkondo wa kwanza, wamesonga mbele kutokana na bao la ugenini dhidi ya City ambao walihitaji ushindi wowote wa tofauti ya mabao mawili.
Mechi ilimalizika kwa mshangao mkubwa kwa mashabiki wa Man-City ambao walikuwa wakishangilia bao la tano ambalo mwamuzi alikataa kulihesabu baada ya kuangalia mtambo wa VAR akidai Raheem Sterling alifunga wakati Sergio Aguero alipokuwa ameotea.
City walitangulia kupata bao la mapema dakika ya nne kupitia kwa Sterling aliyeachilia kombora dakika ya nne akiwa umbali wa mita 15 kutoka lango la Spurs, kabla ya kuongeza la tatu huku mengine yakipatikana kupitia kwa Bernado Silva na Aguero.
Nusura historia hiyo ya Spurs ivurugwe dakika ya mwisho ya mechi hiyo kama si usaidizi wa mtambo wa VAR, kukataa bao la Sterling ambalo kama lingekubalika, lingezima ndoto ya Spurs.
Wakati mashabiki na wachezaji wa City wakishangilia bao la tano ambalo lingewawezesha kutinga nusu-fainali, mtambo wa VAR ulionyesha Aguero alikuwa ameotea wakati bao hilo likiingia wavuni.
Ni mechi ambayo mashabiki walishuhudia mabao matano yakifungwa ndani ya dakika 21, matokeo ambayo yameweka rekodi ya mabao matano yaliyofungwa kwa haraka zaidi katika historia ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kadhalika, ulikuwa ushindi wa kihistoria kwa Spurs ambao hii ilikuwa mara ya kwanza kwao kufuzu kwa nusu-fainali tangu msimu wa 1961-62.
Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettinho alisema: “Ni kama miujiza kwangu jinsi mambo yalivyofanyika uwanjani hapa. Nina furaha tele na ningependa kuwapongeza wachezaji wangu kwa ushindi huo wa ajabu. Nina furaha kwa ajili yao na mashabiki pia.”
Pochettinho sasa anafikia rekodi ya Bill Nicholson ambaye aliiwezesha Spurs kutinga nusu-fainali ya michuano hii msimu wa 1961-1962.
Akizungmza kuhusu mechi hiyo, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alisema walipata nafasi nyingi za kufunga mabao lakini hawakuzitumia vyema, lakini akawapongeza wachezaji wake kwa kujitahidi hadi dakika ya mwisho.
Sasa, Spurs watakutana na Ajax Amsterdam, ambao walishangaza dunia kwa kuibandua nje Juventus kwenye robo-fainali nyingine iliyochezwa Jumanne.
Kwenye nusu-fainali nyingine, Liverpool itakutana na Barcelona baada ya ushindi mkubwa wa 4-1 dhidi ya FC Porto, huku ikifuzu kwa jumla ya mabao 6-1.
Vijana wa kocha Jurgen Klopp walijipatia ushindi huo kutokana na mabao ya Sadio Mane, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Virgil van Dijk. Porto walifunga bao la kufutia machozi kupitia kwa Eder Militao.