Manchester City yapewa idhini ya kuvaana na Real Madrid uwanjani Etihad
Na CHRIS ADUNGO
MCHUANO wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kati ya Manchester City ya Uingereza na Real Madrid ya Uhispania sasa utachezewa ugani Etihad.
Vinara wa mashindano hayo ya soka ya bara Ulaya (Uefa) wamethibitisha kwamba mechi zote za marudiano ya kipute cha UEFA na Europa League zitaandaliwa katika viwanja vya timu za nyumbani bila mahudhurio ya mashabiki.
Man-City watakuwa wenyeji wa Real uwanjani Etihad mnamo Agosti 7 au 8, 2020 huku Chelsea wakisafiri hadi Ujerumani kuvaana na Bayern Munich.
Katika kipute cha Europa League, Wolves watakuwa wenyeji wa Olympiakos huku Manchester United wakivaana na LASK ya Austria mnamo Agosti 5 au 6.
Kampeni za Europa League na UEFA ziliahirishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona baada ya nyingi za mechi za mkondo wa kwanza kusakatwa.
Man-City watashuka dimbani kurudiana na Real wakijivunia ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza ulioshuhudia Chelsea wakipepetwa 3-0 na Bayern uwanjani Stamford Bridge.
Man-United watapepetana na LASK wakijivunia ushindi wa 5-0 katika mkondo wa kwanza ulioshuhudia Wolves wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Olympiakos nchini Uturuki. Rangers watasafiri Ujerumani kurudiana na Bayer Leverkusen wakilenga kujinyanyua kutokana na kichapo cha 3-1 katika mkondo wa kwanza nchini Scotland.
Mechi kati ya Inter Milan na Getafe na nyingine kati ya Sevilla na AS Roma ambazo hazikuwa zimeshuhudia mkondo wa kwanza, sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee na zitachezewa nchini Ujerumani kutokana na hali ya Covid-19 nchini Italia na Uhispania.
Uefa imethibitisha pia kwamba mechi zote kuanzia hatua ya robo-fainali hadi fainali kwenye Europa League na UEFA pia zitachezewa katika viwanja vitupu bila mashabiki.
Mechi za robo-fainali, nusu-fainali na fainali za UEFA zitachezewa zote jijini Lisbon, Ureno kati ya Agosti 12-23, 2020.
Michuano ya raundi tatu za mwisho za Europa League itachezewa katika miji tofauti nchini Ujerumani huku fainali ikiandaliwa mjini Cologne mnamo Agosti 21. Awali, fainali hiyo ilikuwa imepangiwa kuchezewa mjini Gdasnk, Poland.
Kivumbi cha UEFA kwa wanawake kitaendelezwa kwa njia ya mwondoano nchini Uhispania kati ya Agosti 21-30, 2020.