Manchester United watarajiwa kunyanyua Astana
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
BAADA ya msimu mbaya uliopita, Manchester United wamejipata tena katika michuano ya Europa League, siku chache tu kabla ya kuzuru London Stadium kucheza na West Ham United katika pambano la EPL, Jumapili.
Kocha Ole Gunnar anatarajiwa kutumia mechi ya leo Alhamisi dhidi ya Astana kuwajaribu chipukizi kadhaa ambao wamekuwa wakisugua benchi, lakini itakumbukwa kwamba majuzi waliponea chupuchupu dhidi ya Leicester City katika mechi ya EPL.
Mason Greenwood ni miongoni mwa makinda wanaowania kupewa muda wa kutosha uwanjani baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha mchezo akiwa na timu ya vijana na kuifungia mabao 26 katika mechi 30 msimu uliopita. Mchezo wake umefananishwa na wa aliyekuwa staa matata Robin van Persie.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 17 anapigiwa upatu mkubwa wa kuanza kikosini dhidi ya Astana ugani Old Trafford. Huenda pia Angel Gomes akapewa nafasi baada ya kucheza dhidi ya Tottenham wakati wa mechi za maandalizi.
Wengine ni Axel Tuanzebe na Daniel James ambao itakuwa mechi yao ya kwanza ya kiwango cha Ulaya.
Madharau
Hata hivyo, Ole Gunnar Solskjaer hapaswi kuwadharau vijana hao ikikumbukwa kwamba tayari wamefanikiwa kufunga mabao mengi katika mechi za Ligi Kuu nchini Kazakhstan, na kufungwa machache.
Huku wakijivunia nyota walio na uzoevu kama Roman Murtazayev, Marin Tomasov na Dorin Rotariu ambao ni wachezaji wa kimataifa, Astana wanatarajiwa kuzua upinzani mkali.
Hata hivyo, Manchester United wanawekewa matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.