Mashabiki wa Morocco kuandamana dhidi ya FIFA kwa kung'olewa Urusi
Na GEOFFREY ANENE
MOROCCO itacheza mechi dhidi ya Uhispania Jumatatu usiku bila matumaini ya kuingia katika raundi ya 16-bora ya Kombe la Dunia, Kocha Mkuu wa Atlas Lions, Herve Renard, amesema Jumatatu.
Katika mahojiano kabla ya mechi hiyo, ambayo mashabiki wa Morocco wanapanga kuandamana dhidi ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) “kwa kunyimwa penalti tatu dhidi ya Ureno”, Renard amesema hakuna kitu kigumu kama “kucheza mechi unayofahamu kwamba kipenga cha mwisho kikillia utafunganya virago kurejea nyumbani.”
Gazeti la Morocco World News linasema kwamba refa wa mechi kati ya Morocco na Ureno hapo Juni 20, Mwamerika Mark Geiger aliinyima Atlas Lions penalti tatu.
Mbali na kukosa kuipa Morocco penalti, gazeti hilo linadai kwamba, “alikataa kutumia teknolojia ya VAR kuamua ikiwa penalti ya Cristiano Ronaldo ilikuwa halali.”
Mashabiki wa Morocco wamepanga kuonyesha kukerwa kwao na viwango vya usimamizi wa mechi itakapomenyana na mabingwa wa dunia mwaka 2010, Uhispania. Wanapanga kubeba mabango yaliyo na ujumbe maalum wa kukashifu FIFA.
Morocco haina alama katika Kundi B baada ya kufungua kampeni yake kwa kujifunga bao kupitia Aziz Bouhaddouz lililowapa Iran ushindi mwembamba 1-0 Juni 15.
Uhispania na Ureno zinashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama nne kila mmoja nayo Iran ni ya tatu kwa alama tatu. Mechi kati ya Ureno na Iran itachezwa sambamba na ile inayokutanisha Uhispania dhidi ya Morocco.