• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Mashabiki waitaka Ingwe iwagware Rangers kukomesha matokeo duni

Mashabiki waitaka Ingwe iwagware Rangers kukomesha matokeo duni

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa AFC Leopards wameiomba imalize ukame wa mechi nane bila ushindi kwenye Ligi Kuu itakapoalikwa na Posta Rangers uwanjani Afraha mjini Nakuru mnamo Januari 2, 2019.

Ingwe imeandikisha sare dhidi ya Vihiga United (0-0), Sofapaka (2-2) na Kariobangi Sharks (1-1) na kupepetwa 3-0 na Kakamega Homeboyz katika mechi zake nne za kwanza za ligi ya msimu 2018-2019.

Mabingwa hawa mara 13 wa Kenya walifunga msimu 2018 kwa kulazwa na Nzoia Sugar 2-0, Ulinzi Stars 2-1, Tusker 4-0 na Sharks 3-1.

Ushindi wa mwisho wa Leopards katika mechi 11 za ligi zilizopita ni dhidi ya Rangers waliyoilemea 2-1 Septemba 15 kupitia mabao ya raia wa Nigeria Alex Orotomal, ambaye aliondoka msimu huo ulipotamatika.

Mara ya mwisho Ingwe ilizuru Rangers iliambulia alama moja baada ya mechi kumalizika 1-1 Februari 3, 2018.

Rangers inashikilia nafasi ya 14 kwa alama tatu ilizopata kwa kubwaga Mount Kenya Rangers 2-1 Desemba 16. Ilipoteza nyumbani dhidi ya Western Stima (0-1) na Mathare United (1-2). Mathare na Stima ziko bega kwa bega juu ya jedwali kwa alama 10 kila mmoja baada ya kuzoa ushindi mara tatu na sare moja katika mechi zao nne za kwanza. Leopards inashikilia nafasi ya 15 kwenye ligi hii ya klabu 18 kwa alama tatu zilizopatikana kwa kutoka sare dhidi ya Sharks, Sofapaka na Vihiga na kupoteza mikononi mwa Homeboyz.

Shabiki wa Ingwe, Aino L Aino amesema, “Hizi ni alama zetu tatu za kwanza.” Naye Antony Mukonyi alikiri si mechi rahisi. “Ni mechi ngumu sana ya Ingwe, lakini wakitumia vizuri nafasi nyingi ambazo wamekuwa wakiunda, ushindi unaweza kupatikana.” Fanto B Eusebio alikumbusha Ingwe, “Mnakodolea macho kutemwa.”

Ratiba (Januari 2, 2019):

Mount Kenya United na Kariobangi Sharks (2.00pm)

Gor Mahia na Chemelil Sugar (3.00pm)\

Mathare United na KCB (3.00pm)

Nzoia Sugar na Ulinzi Stars (3.00pm)

SoNy Sugar na Kakamega Homeboyz (3.00pm)

Tusker na Vihiga United (3.00pm)

Western Stima na Sofapaka (3.00pm)

Zoo Kericho na Bandari (3.00pm)

Posta Rangers na AFC Leopards (4.15pm)

You can share this post!

Simbas walia kukosa mshahara wa Novemba

NMG yawatuza wauzaji wa magazeti

adminleo