Mashabiki wazidi kutamaushwa na matokeo ya Ingwe
Na GEOFFREY ANENE
MASHABIKI wa AFC Leopards sasa wanajiuliza “timu yetu ilikosea wapi?” baada ya vichapo kuizidi huku ligi ikikaribia kufika katikati.
Ingwe, jinsi timu hiyo inafahamika kwa jina la utani, imeshinda mechi mbili pekee (Posta Rangers 2-0 na Chemelil Sugar 2-1) kati ya 13 imesakata tangu ianze msimu kwa kukabwa 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks mnamo Desemba 9, 2018.
Mabingwa hawa mara 13 wa Kenya wako ndani ya mduara hatari wa kutemwa baada ya kuambulia alama 10 pekee kutoka mechi walizosakata. Walimiminiwa kichapo cha tano mfululizo walipobwagwa 1-0 na Ulinzi Stars katika uwanja wao wa nyumbani wa Kenyatta mjini Machakos mnamo Februari 17. Waliingia mechi hiyo yao ya 13 wakiuguza kupepetwa na Zoo 1-0 (Januari 30), Bandari 4-1 (Februari 3), Mount Kenya United 2-1 (Februari 6) na Gor Mahia 2-0 (Februari 9).
Baada ya kuzamishwa na Ulinzi kupitia bao la Dan Waweru lililopatikana dakika ya tatu, mashabiki wa Ingwe waliudhika na matokeo wakisema inastahili kuwa katika Ligi ya Supa na wala si Ligi Kuu.
Mashabiki Erick Shiakachi na Shikangah Minyata Kevin waliuliza, “Tulikosea wapi?” Babyrich Barasa, “Ingwe itabaki kuwa hadithi tu.” Benard Barasa Romrom, “Tiluraruka….” Joseph Okalama Anyangu, “Upuuzi.” Cornelius Jumbe, “Tuende relegation (Ligi ya Daraja ya Pili) tujipange.”
Matokeo haya duni yanaendelea kuandama Ingwe licha ya wachezaji kurejeshewa mpango wa kuwapata bonasi kutoka Sh3,000 hadi Sh7,000 na pia maafisa timu hiyo kukutana na Waziri wa Michezo Rashid Echesa kutafuta suluhu ya changamoto inapitia. Mnamo Februari 14, 2019, Echesa alitangaza kwamba serikali imepiga jeki Ingwe kwa Sh2 milioni.
Leopards itamenyana na mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United (Februari 23), washindi wa mwaka 2006 SoNy Sugar (Machi 2), mabingwa mara 11 Tusker (Machi 9) na wafalme wa mwaka 2009 Sofapaka (Machi 16) katika mechi zake nne zilizosalia kabla ya ligi hii ya klabu 18 kufika katikati.