• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
MASKINI! Uingereza yalimwa gozi la UEFA Nations League

MASKINI! Uingereza yalimwa gozi la UEFA Nations League

Na MASHIRIKA

GUIMARAES, Ureno

UINGEREZA itaendelea kusubiri zaidi kupata taji lake la kwanza tangu mwaka 1966 baada ya Uholanzi kuibandua kutoka Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya kwa kuichapa 3-1 katika nusu-fainali ya pili katika muda wa ziada mjini Guimaraes, Alhamisi.

Uholanzi sasa itamenyana na wenyeji Ureno, ambao walipatia Uswizi dozi sawia Jumatano, katika fainali itakayochezwa Jumapili.

Penalti ya Marcus Rashford iliipa The Three Lions uongozi wa dakika 45 za kwanza kinyume na mechi ilivyokuwa ikienda, lakini Matthijs de Ligt alirekebisha kosa lake lililochangia kutolewa kwa penalti hiyo kwa kusawazisha 1-1 zikisalia dakika 17 mechi ikatike..

Marcus Rashford iliipa The Three Lions uongozi wa dakika 45 za kwanza kinyume na mechi ilivyokuwa ikienda. Picha/ AFP

Jesse Lingard alidhani amefungia Uingereza bao la ushindi baadaye, lakini lilikataliwa baada ya teknolojia ya VAR kuonesha alirombeza. Waholanzi walitumia kikamilifu fursa ya bao hilo kutohesabiwa kupata mabao mawili ya kuzamisha Uingereza.

Uingereza itajilaumu yenyewe kupoteza mchuano huo baada ya kufanya makosa yaliyozalisha mabao mawili katika muda wa ziada John Stones na Ross Barkley wakiwa wakosaji. Pamoja na bao la kujifunga kutoka kwa Kyle Walker na bao rahisi la Quincy Promes, Uholanzi ilitinga fainali.

Uingereza ya kocha Gareth Southgate ilikuwa ikijaribu kuimarika kutoka nafasi ya nusu-fainali ya kwanza kwenye Kombe la Dunia katika kipindi cha miaka 28 iliyofika mwaka 2018.

Hata hivyo, ilikimbiza vivuli sana uwanjani ishara kwamba itahitaji kufanya mengi kumaliza ukame wa mataji itakapokuwa mwenyeji wa Kombe la Bara Ulaya (Euro) mwaka 2020.

Uholanzi hata haikufuzu kushiriki mashindano mawili makubwa yaliyopita. Hata hivyo, talanta chipukizi iliyoleta mabadiliko makubwa katika jukwaa la kimataifa ilionekana wazi, huku Frenkie de Jong, ambaye anaelekea Barcelona kutoka Ajax, aking’ara katika safu ya kati.

Huku Harry Kane akianzishwa kwenye benchi na Southgate, Rashford alichukua majukumu ya kupiga penalti na akamwaga kipa Jasper Cillessen.

Rashford aliumia kifundo cha mguu katika kabiliano hilo ambalo lilimlazimu apumzishwe baada ya kipindi cha kwanza, huku Kane akijumuishwa kwa dakika 45 za mwisho.

Hata hivyo, mvamizi huyu wa Tottenham Hotspur tena hakuonekana kuwa fiti. Alikuwa ameshiriki fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya mnamo Juni 1 baada ya kupona jeraha lililomweka nje kwa miezi miwili.

Uholanzi ilitawala umilikaji wa mpira, lakini ilikosa makali katika safu ya mbele, Memphis Depay hasa akipoteza nafasi chungu nzima.

Hata hivyo, kujumuishwa kwa Promes na Donny van de Beek kutoka benchini kuliipa Uholanzi nguvu na Uingereza hatimaye iliadhibiwa kwa kucheza sana katika nusu yake pale De Ligt alirekebisha kosa lake kwa kufuma wavuni kona.

Kisha Uingereza ilifanya shambulio zuri, huku Stones, Ben Chilwell, Barkley na Raheem Sterling wakipanga soka safi kabla ya Lingard kujaza kimiani.

Hata hivyo, sherehe za Uingereza zilikatizwa na VAR ilioonyesha kiungo huyu wa Manchester United alifunga bao hilo akiwa ameotea.

Depay alipiga shuti ovyo baada ya shambulio jingine tamu kutoka kwa Uholanzi kabla ya muda wa ziada kutamatika. Uholanzi, hata hivyo, ilitawala kabisa dakika 30 za ziada.

Uingereza ilijidunga mwiba pale Stones alichelewa na mpira na baada ya kipa Jordan Pickford kufanya kazi ya ziada kunyima Depay bao, shuti la Promes liliguswa na Walker na kujaa wavuni.

Pasi hafifu kutoka kwa Barkley kwa kipa wake ilizalisha bao la tatu la Uholanzi baada ya Promes kugonga msumari wa mwisho Depay alipommegea pasi safi.

You can share this post!

Joho, Matiang’i tiketi tosha?

Mtangazaji nguli Mohammed Juma Njuguna amefariki

adminleo