Michezo

Mastaa warejea kikosini kupepetana na Namibia fainali

August 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Dalmus Chituyi, Felix Ayange na Curtis Lilako wamerejea katika kikosi cha Simbas kitakacholimana na Namibia katika fainali ya Kombe la Afrika la raga ya wachezaji 15 kila upande hapo Agosti 18, 2018.

Chituyi, ambaye alipachika miguso miwili katika ushindi wa Kenya wa alama 45-36 dhidi ya Zimbabwe mnamo Juni 30, alikosa mechi dhidi ya Tunisia ambayo Simbas ilitawala 67-0 Agosti 11 jijini Nairobi.

Alikuwa na jeraha sawa na mchezaji wa zamani wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande Ayange, na Lilako.

Kocha Ian Snook anaamini watatu hawa wataleta utofauti mkubwa katika mchezo wa Simbas, ambayo inafukuzia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake.

“Mabadiliko kadhaa tumekuwa tukifanya yamezalisha matunda. Washambuliaji wapya ambao tumetumia kama wachezaji wa akiba wamesababisha tofauti kubwa kila wanapoingia dakika za lala-salama.

Tunatumai mambo pia hayatakuwa tofauti tutakapowatumia wakati huo. Felix ataanza kwenye kiti kwa sababu anaweza kucheza katika nafasi nyingi na kufanya vizuri katika nafasi hizo.

Ni mshindani mkali na tunajua yuko tayari kukabiliana kimwili. Biko Adema, ambaye hucheza nafasi hiyo, bado anauguza jeraha. Curtis amerejea kwa hivyo tunaweza kutumia ujuzi na utulivu wake katika dakika za mwisho mwisho katika mchuano huo.”

Snook pia alizungumzia kuhusu matarajio ya Simbas katika mechi ya Namibia akisema, “Matumaini yetu na azma yetu ni kucheza vyema na katika dakika zote 80.

Tumekuwa tukicheza vyema dakika 40 ama zaidi katika mechi zilizotagulia. Imekuwa vigumu sana kwa sababu hatukuwa na mechi za kujipima nguvu kabla ya msimu kuanza. Mechi ya Tunisia ilitusaidia sana kujaribu karibu kila kitu.

Natumai wachezaji walijifunza kutokana na mechi hiyo. Natarajia kwamba wachezaji wangu wako tayari kutia bidii dakika 80 na wanasubiri mechi hiyo kwa hamu kubwa.”

Simbas, ambayo imepigwa vibaya na Namibia katika safari sita imefanya nchini Namibia, itatoka jijini Nairobi mnamo Jumatano asubuhi kuelekea jijini Windhoek kutafuta kufuta rekodi hiyo duni.

Bingwa wa Afrika ataingia Kombe la Dunia litakaloandaliwa nchini Japan mwaka 2019. Atakutanishwa na New Zealand, Afrika Kusini na Italia pamoja na mshindi wa mchujo wa mwisho, ambaye pia anaweza kuwa Kenya ama Namibia.

Mchujo wa mwisho, ambao utafanyika nchini Ufaransa mwezi Novemba mwaka 2018, utaleta pamoja Canada, Hong Kong, Ujerumani na timu itakayomaliza Kombe la Afrika mwaka 2018 katika nafasi ya pili.

Namibia inaongoza mashindano ya Afrika kwa alama 20. Kenya ni ya pili kwa alama 17. Uganda, Tunisia, Zimbabwe na Morocco zinashikilia nafasi nne zinazofuata kwa alama tisa, nne, tatu na tatu, mtawalia.

Mmoja kati ya Tunisia, Morocco na Zimbabwe atapoteza nafasi katika ligi hii ya daraja ya juu ya Afrika almaarufu Gold Cup. Nafasi yake itajazwa na mshindi wa daraja ya pili almaarufu Silver Cup kati ya Zambia na Algeria.

Kikosi cha Simbas kitakachomenyana na Namibia:

Isaac Adimo (Kenya Harlequin), Martin Owilah (KCB), Samson Onsomu (Impala Saracens), William Ambaka (Kenya Harlequin), Darwin Mukidza (KCB), Tony Onyango (Homeboyz), Peter Kilonzo (KCB), Oliver Mang’eni (KCB), Jacob Ojee (KCB), Mohamed Omollo (Homeboyz), Felix Ayange (Kabras Sugar), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Curtis Lilako (KCB), Peter Karia (KCB), Elkeans Musonye (Strathmore Leos), George Nyambua (Kabras Sugar), Andrew Chogo (Kabras Sugar), Malcolm Onsando (Kenya Harlequin), Patrick Ouko (Homeboyz), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras Sugar), Colman Were (Kabras Sugar) na Davis Chenge (KCB, nahodha).