Michezo

Mataji ya UEFA na Uropa yatatua Uingereza muhula huu

March 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CHRIS ADUNGO

DROO ya robo-fainali za Ligi ya Uropa msimu huu ina maana kwamba Arsenal wanaweza tu kukutana na Chelsea kwenye fainali ya kipute hicho.

Arsenal wana mtihani mgumu wa kuwabandua Napoli katika hatua ya nane-bora ili kujikatia tiketi ya kuvaana na mshindi kati ya Valencia na Villarreal kwenye nusu-fainali.

Kwa upande wao, Chelsea wanapigiwa upatu wa kuwakomoa Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech kirahisi kabla ya kukutana na kikosi kitakachotawala mchuano kati ya Benfica na Eintracht Frankfurt.

Chini ya kocha Maurizio Sarri, Chelsea waliwachabanga Arsenal 3-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Agosti 2018.

Hata hivyo, mkufunzi Unai Emery ambaye pia huu ni msimu wake wa kwanza katika soka ya Uingereza, aliwaongoza Arsenal kulipiza kisasi katika mchuano wa mkondo wa pili ligini. Mabao kutoka kwa Alexandre Lacazette na Laurent Koscielny yaliwapa Arsenal ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Chelsea mnamo Januari 2019.

Kikubwa kitakachofanya mwisho wa kampeni za Ligi ya Uropa kuwa wa kusisimua zaidi msimu huu ni kukutanishwa kwa Chelsea na Arsenal katika fainali iwapo watakosa kumaliza kinyang’anyiro cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora.

Iwapo Manchester United ambao wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer watamaliza kampeni za EPL ndani ya nne-bora, basi njia ya pekee kwa Arsenal au Chelsea kufuzu kwa UEFA msimu ujao ni kunyanyua ubingwa wa Ligi ya Uropa.

Fainali ya kivumbi hicho mwaka huu itaandaliwa jijini Baku, Azerbaijan mnamo Mei 29. Arsenal walidumisha uhai wa kutawazwa mabingwa wa Ligi ya Uropa msimu huu baada ya kuwabandua Rennes kutoka Ufaransa kwa jumla ya mabao 4-3. Vijana wa Emery walipepetwa 3-1 katika mkondo wa kwanza ugenini.

Kwa upande wao, Chelsea waliwabandua Dynamo Kiev kwa jumla ya mabao 8-0 baada ya kuwadhalilisha wenyeji wao wao kwa kichapo cha 5-0 katika mchuano wa mkondo wa pili uwanjani Stamford Bridge.

Arsenal wataanza kampeni zao ugani Emirates huku Chelsea wakitua kwanza ugenini kabla ya kumalizia udhia dhidi ya Prague jijini London. Ni mara ya kwanza kwa wawakilishi wote wa soka ya Uingereza kufuzu kwa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi ya Uropa kwa wakati mmoja.

Liverpool, Manchester City, Manchester United au Tottenham Hotspur wanapigiwa upatu wa kunyanyua taji la UEFA msimu huu. Iwapo Arsenal au Chelsea nao watatwaa ufalme wa Ligi ya Uropa, basi ufanisi huo utarejesha kumbukumbu za 2017-18 ambapo mataji haya mawili yaliwaendea miamba wa soka ya Uhispania.

Katika kampeni za msimu huo, Atletico Madrid waliwazidi maarifa Olympique Marseille katika fainali ya Ligi ya Uropa huku Real Madrid wakiwachabanga Liverpool katika UEFA.

Chelsea walitawazwa mabingwa wa Ligi ya Uropa kwa mara ya mwisho mnamo 2013 huku Emery ambaye ana historia nzuri katika kivumbi hicho akiwaongoza Sevilla ya Uhispania kunyanyua ufalme wa taji hilo mnamo 2014, 2015 na 2016 mtawalia.

Emery, 47, alitua Sevilla baada ya kuagana na Spartak Moscow ya Urusi aliyokuwa ameifunza kwa miezi sita kufikia Januari 2013. Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Sevilla, kocha huyo mzawa wa Uhispania alinyakua taji la Europa League baada ya vijana wake kuwapiga Benfica ya Ureno kwenye fainali.