Michezo

Mathare yapiga Ulinzi na kujihakikishia nafasi ya kusalia KPL msimu ujao

Na CECIL ODONGO May 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MATHARE United Jumamosi ilipiga Ulinzi Stars 1-0 kwenye uga wa Dandora na kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye Ligi Kuu (KPL) msimu ujao.

Vijana wa Kocha John Kamau ambao walirejea KPL msimu huu, walipata bao lao kupitia winga Musa Masika dakika ya 74.

Ushindi huo ulipaisha Mathare, mabingwa wa 2008, hadi nafasi ya 10, kwa alama 40. Hii ina maana kuwa timu hiyo haiwezi kushushwa ngazi kwa kuwa imesalia tu mechi mbili msimu wa 2024/25  utamatike.

Wavuta mkia Bidco United ambao wana alama 29 na Nairobi City Stars ambao wana alama 30 na wamesalia na mechi tatu, hata wakizishinda zote watafikisha tu alama 38 na 39 mtawalia.

Kwa hivyo, hata Mathare ikipoteza mechi zake mbili zilizosalia, haitaweza kushushwa ngazi moja kwa moja kwa sababu haiwezi kufikiwa na City Stars na Bidco.

Timu hiyo sasa inahitaji alama moja pekee kukwepa nafasi ya kushiriki mchujo iwapo Mara Sugar na Murangá Seal ambazo zina alama 32 zitashinda mechi zao zote tatu zilizosalia.

“Ni vyema tumejituma msimu huu na tunalenga ushindi katika mechi mbili zilizosalia ili tumalize kwenye nafasi nzuri. Tulirejea KPL na ni vyema tutaendelea kucheza msimu ujao,” akasema Kamau.

Kwa Ulinzi Stars, msimu huu umekuwa mgumu kwao kwa kuwa wapo nafasi ya 11 kwa alama 37 pia wakiwa wamesalia na michuano miwili msimu utamatike.

Hii leo mbivu na mbichi itabainika wakati ambapo Gor (alama 53) , Kenya Police (alama 58) na Tusker (alama 55) zitakuwa zikivaana na wapinzani hao wakisaka ubingwa wa KPL. Kenya Police na Tusker zimecheza mechi 31 huku nao Gor wakiwa wamecheza michuano 30.

Shabana ambayo ina alama 52 na Kakamega Homeboyz (51) pia zina nafasi finyu za kushinda KPL lakini zitakutana na Kenya Police na Tusker mtawalia kabla ya msimu kukamilika.