Matumaini ya Arsenal UEFA yangali finyu
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
LICHA ya Arsenal kuwapepeta Newcastle United 4-0 na kupaa hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kocha Mikel Arteta amekariri kwamba matumaini ya kufuzu kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao yangali finyu.
Kufikia sasa, Arsenal wanajivunia alama 34, sita zaidi nyuma ya Tottenham waliowachabanga Aston Villa katika dakika za mwisho wa kipindi cha pili na kuchupa hadi nafasi ya tano mnamo mwishoni mwa wiki jana.
Arsenal wamekuwa na panda-shuka tele katika kampeni za EPL muhula huu ambao umewashuhudia wakisajili jumla ya sare 13 na kupoteza mechi sita.
Kufikia wakati kama huu msimu jana, mabingwa hao wa zamani wa soka ya Uingereza walikuwa wakijivunia alama 16 zaidi, matokeo yaliyowadumisha katika nafasi ya nne jedwalini chini ya mkufunzi Unai Emery.
Ingawa hivyo, mwanzo mbaya wa Arsenal katika kipute cha msimu huu ulichangia kutimuliwa kwa Emery na nafasi yake kutwaliwa na Arteta mnamo Disemba 2019. Japo Arsenal wamepoteza mechi moja pekee tangu wakati huo, kikosi hicho kimesajili sare saba chini ya Arteta aliyekuwa msaidizi wa Pep Guardiola kambini mwa Manchester City.
Hadi Arsenal waliposhuka dimbani kumenyana na Newcastle, ni Watford (5) na Norwich City (4) ndivyo vikosi vya pekee vilivyokuwa vimeibuka na ushindi katika michuano michache zaidi ya EPL msimu huu.
Arsenal ambao wamesajili ushindi mara saba kutokana na mechi 26 zilizopita za EPL, wapo katika kundi moja na Crystal Palace, Bournemouth na limbukeni Aston Villa ambao kwa pamoja na West Ham United, Watford na Norwich, wapo katika hatari ya kuteremshwa ngazi msimu huu.
Nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliwafungulia Arsenal ukurasa wa mabao kunako dakika ya 54 baada ya kukamilisha krosi safi ya Nicolas Pepe. Goli hilo la Aubameyang lilikuwa lake la 15 katika EPL msimu huu.
Ushirikiano mkubwa kati ya chipukizi Bukayo Saka na Granit Xhaka ulichangia bao la pili la Arsenal lililofumwa wavuni na Pepe. Mesut Ozil na Alexandre Lacazette ndio waliokizamisha kabisa chombo cha Newcastle United mwishoni mwa kipindi cha pili.
Newcastle ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Palace wikendi hii uwanjani Selhurst Park, wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 31 sawa na Southampton.