MBWEMBWE: Oblak nyani nambari wani anayetamba pia kingwenje
Na CHRIS ADUNGO
JAN Oblak, 27, ni kipa matata mzawa wa Slovenia ambaye kwa sasa anawadakika Atletico Madrid katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Aliingia katika sajili rasmi ya Benfica nchini Ureno akiwa na umri wa miaka 17 pekee na akawa sehemu ya kikosi kilichonyanyua jumla ya mataji matatu katika msimu wa 2013-14.
Alihamia baadaye katika kikosi cha Atletico kwa Sh2 bilioni na kuweka rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi katika soka ya La Liga wakati huo. Slovenia ilimwajibisha kwa mara ya kwanza mnamo 2012.
Anajivunia kuwanyakulia Atletico mataji matatu ya haiba, likiwemo Kombe la UEFA Super Cup mnamo 2018 baada ya kuwapepeta Real Madrid. Chelsea kwa sasa inammezea.
UTAJIRI: Kufikia mwisho wa mwezi jana, Jarida la The Richest lilikadiria ukwasi wa Oblak kufikia Sh4.5 bilioni. Kiini kikubwa cha pato lake ni mshahara wa yapata 44 milioni ambao hupokezwa na Atletico mwishoni mwa kila wiki uwanjani Wanda Metropolitano.
Mbali na ujira huo ambao unafikia takriban Sh178 milioni kwa mwezi, Oblak hujirinia hela nyinginezo kutokana na kuwa balozi wa matangazo wa kampuni mbalimbali au marupurupu ya kusajili ushindi katika mechi za ngazi ya klabu na timu ya taifa.
Malipo ambayo kwa sasa anapokezwa na Atletico yanamfanya sogora anayedumishw akwa mshahara mkubwa zaidi kambini mwa Atletico. Kimshahara, mgongo wake unasomwa kwa karibu na Diego Costa, Jorge Koke, Joao Felix na Saul Niguez.
Mnamo Aprili 2019, Oblak alitia saini mkataba mpya wa miaka minne katika makubaliano yatakayomshuhudia akipokezwa na Atletico ujira wa Sh44.8 milioni kwa wiki hadi Juni 2023.
Anashikilia nafasi ya nane miongoni mwa makipa ghali zaidi duniani kwenye orodha inayoongozwa na mlinda-lango wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga. Oblak anawafuata kwa karibu sana makipa Alisson Becker (Liverpool), David De Gea (Man-United), Hugo Lloris (Tottenham Hotspur), Thibaut Courtois (Real Madrid), Ederson Moraes (Man-City) na Marc-Andre ter Stegen (Barcelona).
MAKASRI: Oblak anamiliki majumba ya fahari jijini Madrid, Uhispania. Anaishi katika kasri ambalo thamani yake inakadiriwa kufikia Sh600 milioni. Mnamo 2014, utajiri wa Oblak katika umri wake mdogo ulichangia kuvamiwa kwake na majambazi waliompora mali ya thamani kubwa isiyojulikana. Aliwajengea wazazi wake Matjaz na Stojanka Majkic makazi ya kifahari na majumba ya kibiashara katika majiji ya Ljubljana na Maribor mnamo 2017.
MAGARI: Oblak anamiliki magari mengi ya haiba kubwa. Miongoni mwa michuma anayosukuma ni Volkswagen GTI, Audi S8, Jaguar XJ, Bentley Continental GT, Aston Martin na Ford F150. Magari haya yote yanakisiwa kumgharimu Sh156 milioni.
FAMILIA na MAPENZI: Oblak alizaliwa mnamo Januari 7, 1993 viungani mwa mji wa Skofja Loka, Slovenia. Dada yake mkubwa, Teja, ni mwanavikapu maarufu ambaye kwa sasa huchezea timu ya taifa ya Slovenia. Ingawa safari yake ya mahusiano ni siri, Oblak aliwahi kuhusishwa kimapenzi na mwanamitindo Kathrin Glich aliyekuwa akimburudisha kipa na nahodha wa Bayern Munich, Manuel Neuer