Messi achezea Barcelona kwa mara ya kwanza tangu kuhama kwake kutibuke
Na MASHIRIKA
LIONEL Messi, 33, alichezea Barcelona kwa mara ya kwanza tangu jaribio lake la kuagana na miamba hao wa soka ya Uhispania kugonga mwamba.
Fowadi na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina, aliwajibishwa na kocha mpya Ronald Koeman katika mechi ya kirafiki iliyokutanisha Barcelona na Gimnastic de Tarragona.
Messi aliwawasilishia vinara wa Barcelona ombi la kutaka kubanduka ugani Camp Nou mnamo Agosti 2020 ila akaamua kusalia kambini mwa kikosi hicho kwa kuwa hakukuwa na klabu iliyokuwa radhi kuweka mezani Sh89 bilioni ili kumsajili kwa mujibu wa kifungu kilichokuwa kwenye mkataba wake.
Messi alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Barcelona ambao wamethibitisha kwamba nyota huyo atasalia kuwa nahodha wao. Aliondolewa ugani mwishoni mwa kipindi cha kwanza na nafasi yake kutwaliwa na Ousmane Dembele aliyefungua ukurasa wa mabao.
Magoli mengine ya Barcelona yalifumwa wavuni kupitia penalti za Antoine Griezmann na Philippe Coutinho.
Yalikuwa matamanio ya Messi kutumia kifungu kilichomkubalia kuondoka ugani Camp Nou mwishoni mwa msimu huu kukatiza uhusiano wake na Barcelona.
Barcelona wamepangiwa kuanza kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Septemba 27, 2020, dhidi ya Villarreal ugani Camp Nou.