Messi anakaribishwa sana PSG – kocha Thomas Tuchel
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Thomas Tuchel wa Paris Saint-Germain (PSG) amesema atakuwa mwingi wa fahari kumkaribisha nyota Lionel Messi kambini mwake iwapo fowadi na nahodha huyo wa Argentina atahiari kuagana rasmi na Barcelona nchini Uhispania.
Hata hivyo, Tuchel anahisi kuwa itakuwa vigumu mno kwa Messi kuagana na waajiri wake wa sasa.
Messi, ambaye alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 pekee, amefungia Barcelona jumla ya mabao 634 kutokana na mechi 730 zilizopita na ndiye mwanasoka anayejivunia historia ya mafanikio makubwa zaidi ugani Camp Nou.
Sogora huyo mwenye umri wa miaka 33 yuko katika mwaka wake wa mwisho kwenye mkataba wake na Barcelona ambao amewanyanyulia jumla ya mataji 33.
Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, mustakabali wa Messi kambini mwa Barcelona bado unaning’inia pembamba baada ya Barcelona kudhalilishwa 8-2 na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Aidha, kikosi hicho kilikamilisha kampeni za 2019-20 bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2013-14 baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kubanduliwa mapema na Athletic Bilbao kwenye kivumbi cha Copa del Rey.
Mbali na PSG, Messi anahusishwa pakubw ana uwezekano wa kutua kambini mwa Juventus, Inter Milan au Manchester City ambapo ataungana na kocha wake wa zamani kambini mwa Barcelona, Pep Guardiola.
“Anakaribishwa sana PSG. Ni kocha yupi duniani ambaye hatataka kuwa na Messi kambini mwake?” akatanguliza Tuchel.
“Hata hivyo, sioni akiagana na Barcelona. Nadhani atastaafu akivalia jezi za kikosi hicho. Ndiye Bw Barcelona hasa!” akasema mkufunzi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ambaye chini yake, PSG walipigwa 1-0 na Bayern kwenye fainali ya UEFA msimu huu jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 23, 2020.
Tuchel amefichua mipango ya kujishughulisha pakubwa katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu kadri PSG wanavyojitahidi kujaza mapengo ya wanasoka Thiago Silva na Eric Maxim Choupo-Moting.
“Tulipoteza wanasoka wengi sana mwanzoni mwa msimu huu, na bado tutaagana na wengine wawili hivi punde. Ipo haja ya kujisuka upya kwa minajili ya msimu ujao ambao una malengo mapya na makubwa zaidi,” akaongeza kocha huyo mzawa wa Ujerumani.
PSG walitawazwa mabingwa wa mataji matatu msimu huu – Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), French League Cup na French Cup.