Michezo

Minnaert afurushwa Rwanda kwa matokeo ya aibu

June 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA kocha AFC leopards Ivan Minnaert ametimuliwa na waajiri wake Klabu ya Rayon Sports ya Rwanda kufuatia misururu ya matokeo mabaya.

Minnaert ambaye ni raia wa Ubelgiji anatambuliwa kwa kuiongoza Rayon Sports kushiriki michuano ya Kombe la mashirikisho baada ya kubanduliwa na Mamelodi Sudowns ya Afrika Kusini katika kipute cha kuwania klabu bingwa barani Afrika.

Kocha huyo alikuwa akihudumia Rayon Sports baada ya kuagana nao mwaka wa 2016 na kujiunga na wapambe wa soka nchini Kenya AFC Leopards kisha akarejea kuwawajibika baada ya kuachishwa kazi na mabingwa hao mara 12 wa KPL.

Kocha huyo ametimuliwa baada ya kukosana na wengi wa wachezaji katika kikosi cha kwanza wanaosemekana kumgomea na hata kumchongea kupitia kusakata gozi vibaya kimaksudi ili wasajili matokeo mabaya ndipo amwage unga.

‘‘Kocha mkuu wa Rayon Sports Ivan Minnaert si kocha mkuu tena, ametimuliwa kutokana na matokeo mabaya na kukosa uhusiano mzuri na wachezaji. Manaibu wake Jeanot Witakenge na Marcel Lomami pia wamesimamishwa kazi kwa muda hadi klabu itakapotoa habari zaidi kuwahusu,” ikasema taarifa ya Klabu hiyo.

Rayon Sports wanashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa jedwali la ligi ya Rwanda jambo linalodaiwa kusababishwa na matokeo yasiyoridhisha chini ya uongozi wa kocha Minnaert.

Katika michuano ya kuwania ubingwa wa kombe la mashirikisho, Rayon Sports wananing’inia katika nafasi ya tatu kwenye kundi linalojumiusha mabingwa wa Kenya Gor Mahia, Yanga ya Tanzania na USM Algier kutoka Algeria. Wamesajili sare mbili na kichapo mikononi mwa USM Algier.

Mkufunzi huyo aliagana na Ingwe mwezi Septemba mwaka 2016 na kurejea Rayon Sports baada ya kuwajibikia washiriki wa ligi ya Rwanda Mukura VS.