• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Miti milioni 19 kupandwa kwa ajili ya Safari Rally

Miti milioni 19 kupandwa kwa ajili ya Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed amefichua kuwa Kenya inapanga kupanda miti milioni 19 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuadhimisha kurejea kwa Safari Rally ambazo hazikuwa kwenye kalenda ya Mbio za Magari za Dunia (WRC) kwa kipindi cha miaka 19.

Akizungumza katika hafla moja ya mbio za Safari Rally mjini Mombasa, Mohamed alisema, “Kwa sababu Safari Rally haikufanyika mwaka huu (2020) kutokana na janga la virusi vya corona, natumai tutabadilisha idadi ya miti tulipanga kupanda kutoka milioni 18 kuwa milioni 19 ili kuadhimisha miaka 19 ambayo Safari Rally haikuwa kwenye ratiba ya WRC.”

“Lengo letu ni kupanda miti milioni 1.9 mwaka huu. Mradi huu utahusisha maeneo ambayo yameharibiwa kutokana na ukataji wa miti, sehemu ambazo mbio za Safari Rally zimekuwa zikitumiwa na pia zile za Shirikisho la Mbio za Magari Kenya, maeneo ya kurekebishia magari yanayoshiriki mbio za magari na pia sehemu zinazotumiwa na mashabiki wakati wa mbio za Safari Rally katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.”

Waziri huyo alifafanua kuwa mradi huo utafanywa kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira na Misitu, Huduma za Misitu ya Kenya (KFS), Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) na mradi wa kulinda mito (Save Our Rivers Initiative).”

Amina pia alifichua kuwa serikali inashirikiana na wataalamu mbalimbali kuanzisha mradi muhimu kuhusu usalama barabarani utakaotilia mkazo maadili ya mashindano salama.

Waziri huyo, ambaye majuzi aliteuliwa kuhudumu katika paneli ya juu ya Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA) inayohusika na usalama barabarani, pia alisema kuwa Kenya inaunga mkono kampeni ya FIA ya kudumisha usalama barabarani, huku maandalizi ya Safari Rally 2021 yakiwa yamepamba moto.

Alisema wizara yake imeungana na Chama cha Kunadi na Kulinda maslahi wa madereva Kenya (AA) ambacho ni mwanachama wa FIA.

Waziri huyo pia alifichua kuwa kuna mipango ya wizara yake kushirikiana na Halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani (NTSA) kufundisha kizazi kijacho cha madereva masuala ya usalama barabarani, miongoni mwa miradi mingine.

Waziri Amina, ambaye atahudhuria mkutano wa paneli ya usalama barani wa FIA hapo Oktoba 28 mjini Monaco, pia alifichua kuwa kuna mipango ya kualika nchini Rais wa FIA Jean Todt. Todt pia ni Afisa Maalum wa Usalama Barabarani kwenye Umoja wa Mataifa.

Safari Rally ilikuwa kwenye ratiba ya WRC kutoka mwaka 1973 hadi 2002 kabla ya kuondolewa kutokana na ukosefu wa ufadhili kutoka kwa serikali. Duru hiyo ilifaa kurejea mwaka 2020 baada ya Kenya kufaulu katika ombi lake la kujumuishwa tena kwenye WRC, lakini mkurupuko wa virusi vya corona ulifanya iahirishwe hadi mwaka 2021. Itafanyika Juni 24-27, 2021.

You can share this post!

Katiba: Uhuru, Raila kuongoza ukusanyaji sahihi

Klabu anayochezea Mkenya Arnold Origi yafufua matumaini ya...