• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
MNADANI: PSG wamshiba Neymar, tayari kabisa kumuuza

MNADANI: PSG wamshiba Neymar, tayari kabisa kumuuza

Na MASHIRIKA

BRASILIA, Brazil

MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG), Leonardo Araújo amesema klabu hiyo itampiga bei Neymar baada ya nyota huyo kukosa kufika kambini kwa mazoezi.

Neymar alitarajiwa kufika kambini Jumatatu lakini hakuonekana huku kukiwa na uvumi kwamba staa huyo anapanga kurejea katika klabu yake ya zamani ya Barcelona.

Alipoulizwa iwapo ana hakika mchezaji huyo wa miaka 27 anapanga kuondoka, Leonardo alisema, “Kila mtu anafahamu hilo. Lakini katika soka, mtu husema kitu leo na kubadilika kesho. Nilizungumza naye pamoja na washirika wake. Kila mtu anafahamu anavyofikiria.

“Kumbukeni tuna mkataba wa miaka mitatu naye. Na kwa kuwa hatujapokea ofa yoyote, hakuna tunachoweza kuzungumza kwa sasa. Hatujapata ofa kutoka kwa klabu yoyote, lakini tumekuwa tukisikia mambo mengi kuhusu anavyotaka.”

Barcelona wamesema wanataka kumnunua lakini kuna masharti. Ni rais Joseph Maria wa Barcelona mwenyewe aliyesema hayo. Lakini hatujapata mawasiliano rasmi. Kuondoka kwa mchezaji muhimu kama yeye sio jambo la kuchezea. Ni uhamisho unaohusu kiasi kikubwa cha pesa.

“Neymar anaweza kuondoka PSG, sikatai, lakini lazima utaratibu unaofaa ufuatwe. Lakini kufikia sasa hakuna chochote tulichopokea kuhusu uvumi huo, hatuna uhakika kama kuna mtu anayetaka kumsajili, wala kiasi kilichotengwa kumtwaa. Mambo kama haya hayafanywi kwa siri, hilo mwalifahamu.

“Kwa sasa tunaangalia wachezaji walio kambini kwa ajili ya msimu ujao. Hatupotezi nafasi kwa watu walio mbali.”

Taarifa ya klabu ilisema, Mchezaji Neymar Jr alitarajiwa kufika kambini Jumatatu lakini hajaonekana kufikia sasa. Klabu haijawasiliana naye wala hajapewa likizo. Tunasikitishwa na habari hizi na tutawasiliana nanyi baadaye.”

Hata hivyo, Leonardo hakueleza iwapo klabu hiyo itamchukulia hatua staa huyo mwenye umri wa miaka 27, ila tu alisema utaratibu unaofaa utafuatwa kwa makini. Neymar alijiunga na PSG akitokea Barcelona kwa Sh26 bilioni mnamo 2017.

Neymar alikosa kucheza michuano ya Copa America kutokana na jeraha linalomtatiza.

Timu yake ya Brazil ilibeba ubingwa wa mechi hizo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Peru mnamo Jumapili kwenye fainali.

Nyota huyo aliyeumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya Qatar kabla ya kuanza kwa Copa America, amepigwa marufuku ya mechi tatu za Ligue 1 baada ya kumshambulia shabiki mwezi Aprili baada ya fainali ya French Cup dhidi ya Rennes ambayo walipoteza.

Kadhalika mchezaji huyo wa zamani wa Santos atazikosa mechi tatu za Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) baada ya kumfokea mwamuzi walipokuwa wakicheza na Manchester United, msimu uliopita.

You can share this post!

Kocha Genot Rohr awataka vijana wake kuepuka makosa...

Wiper kutangaza mwenyekiti mpya mwishoni mwa Julai

adminleo