Mourinho atilia shaka uzalendo wa baadhi ya wanasoka wake Tottenham
Na MASHIRIKA
KOCHA Jose Mourinho ametilia shaka kiwango cha uzalendo, uaminifu na kujitolea kwa baadhi ya wachezaji wake baada ya kikosi chake cha Tottenham Hotspur kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya LASK kwenye mechi ya Europa League iliyosakatiwa nchini Austria mnamo Disemba 3, 2020.
Licha ya matokeo hayo, Tottenham walifuzu kwa hatua ya 32-bora ya kivumbi hicho. Ilikuwa mara ya kwanza kwa kikosi hicho kufungwa mabao matatu tangu waambulie sare ya 3-3 dhidi ya West Ham United kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 2020.
Dele Alli alitokea benchi na kuwaweka Tottenham kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 86 kabla ya Mamoudou Karamoko, aliyemtatiza sana kipa Joe Hart, kusawazisha mambo sekunde chake kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano kupulizwa.
Gareth Bale aliwafungulia Tottenham ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia penalty baada ya Peter Michorl kuwaweka LASK uongozini katika dakika ya 42. Bao la pili la Tottenham lilifumwa wavuni na fowadi Son Heung-min katika dakika ya 56 kabla ya juhudi zake kufutwa na Johannes Eggestein katika dakika ya 84.
“Ni tatizo la dhana na mtazamo mbaya kutoka kwa wachezaji wetu. Niliwahi kushuhudia hali sawa na hii kwa sasa wakati nikiwanoa wanasoka wa Manchester United ambao walipoteza mechi mbili za ugenini kwenye hatua ya makundi ya Europa League,” akasema Mourinho ambaye ni mzawa wa Ureno.
“Tukifika kwenye hatua ya mwondoano ambapo kila kikosi kimejiandaa vilivyo, basi itakuwa vigumu kusonga mbele iwapo wachezaji watasalia na mtazamo walioudhihirisha dhidi ya LASK,” akatanguliza Mourinho.
“Ni dhana mbaya sana kwa wachezaji wa Tottenham kufikiria kwamba mechi makundi katika Europa League si muhimu na wapo wanasoka fulani tu ambao kazi yao ni kushiriki mechi za kipute hicho,” akaeleza Mourinho ambaye pia amewahi kunoa Inter Milan, FC Porto, Real Madrid na Chelsea.
Chini ya Mourinho, Tottenham walipigwa 1-0 na Royal Antwerp nchini Ubelgiji mnamo Oktoba kabla ya kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Ludogorets ugenini mnamo Novemba 2020.
Ingawa Tottenham tayari wamefuzu kwa hatua ya 32-bora kwenye Europa League msimu huu, watalazimika kupiga Antwerp katika marudiano ya Disemba 10, 2020 jijini London, Uingereza ili wajipe uhakika wa kutua kileleni mwa Kundi J.
Tottenham kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kundini kwa alama 10, mbili nyuma ya viongozi Antwerp. LASK wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama saba huku Ludogorets wakivuta mkia bila alama yoyote.