Michezo

Mpango wa Real Madrid kumsajili Mbappe hautaathiriwa Zidane akiondoka – Klabu

October 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHARIKI

MAAZIMIO ya Real Madrid kumsajili chipukizi Kylian Mbappe kutoka Paris Saint-Germain (PSG) mwishoni mwa msimu huu hayatazimwa hata endapo kocha Zinedine Zidane atatimuliwa.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Real huenda wakampiga Zidane kalamu wakati wowote baada ya kumzungumzia Mauricio Pochettino na nyota wao wa zamani Raul Gonzalez kuhusu uwezekano wa kutwaa mikoba yao.

Real ambao ni mabingwa mara 13 wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) walidhalilishwa kwa kichapo cha 3-2 kutoka kwa Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwenye kivumbi hicho mnamo Oktoba 21 siku chache baada ya masogora wa Zidane kupepetwa 1-0 na limbukeni Cadiz kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Real watakuwa wageni wa Barcelona katika gozi la El Clasico mnamo Oktoba 24 uwanjani Camp Nou katika mechi ambapo Zidane ana ulazima wa kuongoza wanasoka wake kusajili ushindi ili kuweka hai matumaini ya kuendelea kuwa mkufunzi wa miamba hao wa Uhispania na bara Ulaya.

Iwapo Real watamtema Zidane kwa sababu ya matokeo duni, usimamizi umeshikilia kwamba tukio hilo halitaathiri kwa vyoyote mpango wa Mbappe kutua ugani Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu huu.

“Si siri kwamba Zidane anawania nafasi ya kumsajili Mbappe, 21. Anaamini kwamba Mbappe ndiye nyota atakayeweka hai matumaini ya Real kutwaa mataji zaidi ya UEFA,” ikasema sehemu ya taarifa kwenye gazeti la Mundo Deportivo.

“Kwa yote mazuri ambayo nimejinyakulia nikichezea timu ya taifa ya Ufaransa na Real Madrid. Kisha akaja Cristiano Ronaldo ambaye alifanya kazi kubwa ugani Santiago Bernabeu. Hata hivyo, wawili hao wameacha alama ya kudumu na kumbukumbu nzuri kambini mwa Real. Sasa ni fursa ya Zidane kuweka historia mpya katika ngazi nyingine kambini mwa Real,” ikaendelea taarifa hiyo.

Mkataba kati ya Mbappe na PSG unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa 2022 tangu ajiunge rasmi na miamba hao wa soka kutoka kambini mwa AS Monaco mnamo 2017 kwa kima cha Sh23 bilioni.

Mnamo Septemba 13, 2020, Mbappe aliwaarifu PSG kuhusu matamanio yake ya kuagana nao mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21 ili ajiendeleze zaidi kitaaluma kwingineko.

Akiwa shabiki sugu wa Liverpool, Mbappe anapigiwa upatu wa kutua Uingereza kuvalia jezi za miamba hao wa Ligi Kuu ya EPL au kuyoyomea Uhispania kuchezea Real Madrid ambao wamekuwa wakimvizia kwa muda mrefu uliopita.

Usajili wake ndio ghali zaidi kwa chipukizi na unasalia kuwa wa pili ulio ghali zaidi katika historia ya soka baada ya ule wa Sh28 bilioni uliomshuhudia fowadi Neymar Jr akimbanduka kambini mwa Barcelona na kutua PSG mnamo 2017.

Mbappe ambaye pia amekuwa akihusishwa na Manchester City na Liverpool kwa kipindi kirefu, alitia saini kandarasi rasmi ya miaka mitano na PSG mnamo 2018 na akafungia kikosi hicho jumla ya mabao 29 kutokana na mechi 33 za msimu wa 2019-20.