Michezo

Mshambuliaji Harry Kane adhamini jezi za kikosi cha Leyton Orient msimu ujao

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

NAHODHA wa timu ya taifa ya Uingereza na klabu ya Tottenham Hotspur, Harry Kane, amedhamini jezi za kikosi chake cha zamani cha Leyton Orient kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Kane, 26, aliwajibishwa katika kikosi cha watu wazima kambini mwa Orient kwa mara ya kwanza mnamo 2011.

Kwenye mikono ya jezi hizo, maandishi ya kuwapongeza maafisa wa afya wa hospitali ya Mind and Haven House Children’s Hospice, Uingereza yataandikwa katika hatua ya kutambua juhudi zao katika kupambana na janga la corona. Nembo ya hospitali hiyo itatiwa pia kwenye sehemu ya kifua ya jezi, karibu na ilipo nembo ya klabu ya Orient.

Kane alikuwa na umri wa miaka 17 pekee alipoingia katika sajili rasmi ya Orient kwa mkopo kutoka Tottenham. Katika kipindi hicho cha mkopo, alipachika wavuni jumla ya mabao matano kutokana na mechi 18 kabla ya kurejea Tottenham ambapo nyota yake ilianza kung’aa zaidi kitaaluma.

Orient wamesema kwamba asilimia 10 ya fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya jezi zao zitatiwa kwenye hazina ya Hospitali ya Mind and Haven House Children’s Hospice.

“Nilizaliwa na kukulia karibu na uwanja wa kikosi cha Orient kilichonipokeza malezi ya awali kabisa katika ulingo wa soka. Ninajivunia sana fursa hii ya kurejesha hisani yangu kwa jamii, na hususan kikosi kilichotambua utajiri wa kipaji changu na kunipa fursa ya kukidhihirishia ulimwengu mzima,” akatanguliza Kane.

“Klabu hii pia imenipa jukwaa mwafaka zaidi la kutoa pongezi zangu kwa maafisa wa afya waliopo mstari wa mbele kukabiliana na janga la corona kwa njia ya kipekee. Wamejitolea kwa moyo wote kuwahudumia waathiriwa na kuwarejeshea matumaini ya kuishi katika kipindi hiki kigumu chenye changamoto tele,” akasema.

“Kilichoanza kama wazo dogo tu la kawaida kwa sasa limekuwa suala kubwa ambalo limetupa mdhamini wa jezi kwa msimu mzima. Asante sana Kane; wewe ni kielelezo chema na pongezi nyingi ziwafikie wahudumu wetu wa afya kwa kujinyima kiasi hicho,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Orient, Danny Macklin.