Michezo

Mtambue chipukizi Eddie Nketiah wa Arsenal!

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KIJANA Edward “Eddie” Keddar Nketiah ni mmoja wa wachezaji wanaoinuka kwa haraka katika kambi ya Arsenal kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mshambuliaji huyu Muingereza alimiminiwa sifa na kocha Mikel Arteta kwa kutandaza soka ya kuvutia dhidi ya Sheffield United juma moja lilopita kwenye Kombe la FA.

Kiwango chake cha mchezo kwenye mechi hiyo pia kulimfanya Mfaransa Alexandre Lacazette, 29, kuzinduka kutoka usingizini.

Safari ya Nketiah kuwa mwanasoka haijakosa mabonde. Chipukizi huyu aliye na asili ya Ghana alizaliwa Mei 30, 1999 katika mtaa wa Lewisham jijini London.

Ni mtaa ambao pia anatokea jagina wa Arsenal, Ian Wright na vile vile kiungo wa Chelsea, Ruben Loftus-Cheek.

Kitindamimba huyu alianza kusakata soka utotoni akicheza na babake nyumbani na pia watoto wenzake.

Alionwa na maskauti ambao walimsajili katika akademia ya Chelsea mwaka 2008 baada ya kufanyiwa majaribio na kupita.

Nketiah, 21, alicheza bega kwa bega na nyota wengine wachanga wa Chelsea, kama Mason Mount na Callum Hudson-Odoi.

Mchezo wake ulilinganishwa na ule wa mshambuliaji mzoefu Jermain Defoe, hasa kutokana na alivyokuwa akizunguka uwanja na pia kusukumia makipa makombora moto moto kutoka pembe zote.

Hata hivyo, kinda huyu alipata pigo alipotupwa nje ya akademia ya Blues mnamo 2015 baada ya kukosolewa mara kadhaa kwa kukosa nguvu anazostahili kuwa nazo kama mshambuliaji.

Kwa bahati nzuri, familia yake na marafiki wa karibu walisimama naye na kumuepushia msongo wa mawazo anaopata mtu anapokataliwa. Hata hivyo, hakusahau kwa haraka masaibu hayo.

Familia yake ilielewa ari yake ya kutaka kuwa mwanasoka wa kulipwa. Hali hii ilimsukuma babake kumuulizia nafasi katika akademia nyingine.

Bisha bisha za mzazi zilizaa matunda muda si mrefu Nketiah alibahatika kupewa fursa na Arsenal, ambayo ilikubali kumlipia karo ya kukuza soka yake wiki mbili tu baada ya Chelsea kumtupa nje.

Tangu aingie akademia ya Arsenal, chipukizi huyu hajalegeza kamba. Aliimarika na kuimarika, akichochewa na msukumo aliokuwa nao wa kufanya soka kuwa kazi yake ya kila siku. Kazi yake iliridhisha makocha.

Haikumchukua Nketiah muda kabla ya kuisaidia Arsenal kushinda Ligi Kuu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21 (U-21).

Akafungia timu ya wachezaji wasiozidi miaka 18 (U-18) mabao 15 katika mechi 16, pamoja na ile ya wachezaji wasiozidi miaka 23 (U-23) mabao 12 katika michuano 26 msimu wa 2016-2017.

Kutokana na bidii yake, kocha Arsene Wenger alimjumuisha katika ziara ya Australia na Uchina kujiandaa kwa msimu mpya. Alishiriki mechi yake ya kwanza kabisa kwenye Ligi ya Uropa dhidi ya BATE Borisov ambayo Arsenal ilitawala 4-2.

Hatua nyingine muhimu katika taaluma yake ilikuwa mwaka 2018 aliposaidia Uingereza kunyakua taji la Toulon akishirikiana na wachezaji kama Kyle Walker-Peters, Fikayo Tomori na Tammy Abraham. Mafanikio hayo yalimsaidia kurejesha sifa yake na kujiamini.

Nketiah anasema soka yake pia imepata mwelekeo mzuri kwa kuwaenzi washambuliaji wa zamani wa Arsenal, Ian Wright na Thierry Henry.

Alianza msimu huu wa 2019-2020 kwa mkopo katika kikosi cha Leeds United kwatika Ligi ya Daraja ya Pili (Championship).

Hata hivyo, ujasiri wake katika mechi 17 alizochezea Leeds, kasi aliyokuwa nayo pamoja na uwezo wa kukamilisha mashambulizi ulifanya Arteta kumrejesha uwanjani Emirates mwezi Januari.

Tangu arudi nyumbani amecheza mechi nane za ligi EPL ikiwemo dhidi ya Southampton hapo Juni 25 alipochangia bao moja katika ushindi wa magoli 2-0 uwanjani St Mary’s.

Nketiah anapokea mshahara wa Sh1.9 milioni kila wiki, kutoka Sh265,000 alizokuwa akipokea miaka miwili iliyopita.