Muhiddin aelezea matumaini ya Bandari kung’aa KPL, FKF
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
MASHABIKI wa soka wa eneo la Pwani, wamehakikishiwa kuwa timu ya Bandari itafanya vizuri kwenye mechi zao zijazo.
Hii ni baada ya timu hiyo kwani kuanza harakati za kujirekebisha kwa makosa yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ilipocheza na Gor Mahia ugenini. Ilifunga mabao 3-0 uwanjani Afraha mjini Nakuru.
Akiongea Jumanne na ‘Taifa Leo’ wakati wa timu yake ilikuwa kwa mazoezi katika uwanja wao wa Mbaraki Sports Club, kocha Twahir Muhiddin, alisema anafanya kazi ya kurekebisha makosa.
Timu hiyo alieleza inalenga kujirekebisha watakapokutana na Posta Rangers mjini Machakos wikiendi hii.
“Nafanyia kazi makosa madogo yaliyofanyika huko Nakuru ili tuweze kucheza vizuri zaidi tutakapopambana na Rangers. Ninaamini wachezaji wangu mara hii watatumia nafasi watakazopata za kufunga mabao,” akasema Muhiddin.
Mkufunzi huyo wa Bandari ameeleza wapenzi wa timu hiyo watarajie mazuri kwenye mechi zijazo za Ligi Kuu ya Kenya (KPL), na mashindano ya Kombe la FKF.
“Kushindwa kwa mabao 3-0 na Gor Mahia, si kuwa wachezaji wetu hawakucheza vizuri. Wanasoka wetu walicheza vizuri lakini haikuwa siku nzuri kwetu kwani mastraika wetu walikosa nafasi zisizopungua sita za wazi,” akasema Muhiddin.
Alisema wachezaji wake walicheza mtindo mzuri ambao watautumia kwenye mechi yao ijayo.
“Tatizo letu kubwa lilikuwa makosa ya wachezaji binafsi ya kupoteza nafasi nzuri za kufunga ambazo zilikuwa zaidi ya asilimia 50,” akasem Muhiddin.
Alisema anafanya kazi kurekebisha makosa madogo ili wachezaji wasirudie makosa waliyoyafanya dhidi ya Gor. Pia analenga kuona kuwa timu inarudia hali yake nzuri na kupata ushindi.
“Nina imani wachezaji watajirekebisha tuweze kupata ushindi mechi zetu zijazo,” akasema Muhiddin.
Matokeo ya mechi ya Bandari kuchapwa mabao 3-0 na Gor, yameibua maoni tofauti kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ya Pwani ambayo ndiyo pekee inayoshiriki ligi ya KPL.
Makosa madogo
Wengine wanasema timu ilifanya makosa madogo yanayoweza kurekebishwa ilhali wengine wakilaumu timu kwa kucheza kwa njia isiyofaa.
Baadhi ya mashabiki wanaona Bandari inaweza kuwa mojawapo ya timu bora zaidi barani Afrika Muhiddin akiendelea kuiandaa timu hiyo.
“Tumefungwa na Gor lakini mchezo tuliocheza ulikuwa wa hali ya juu,” alisema Juma Said wa Mombasa.
Lakini mashabiki wengine wangali wanadai Bernard Mwalala alifaa kuendelea kuiandaa timu hiyo sababu ilikuwa imeanza kurudia hali iliyokuwa.
“Sikuona sababu ya Mwalala kuwekwa kando ilhali timu ilianza kurudia hali yake ya ushindi,” akasema Ronald Maneno.