MUUJIZA: Reds yatenda muujiza Uefa
BARCELONA walikuwa wameduwaa, Liverpool hawaamini nao mashabiki wakawa na hisia mseto baada ya filimbi ya mwisho ya mechi ya nusu fainali, duru ya pili, baina ya mabingwa wa Uhispania na miamba wa Uingereza mnamo Jumanne uwanjani Anfield, Uingereza.
Matokeo yalikuwa 4-0 kwa fahari ya Liverpool, hii ikimaanisha vijana hao wa Jurgen Klopp walikuwa wamepindua kipigo cha 3-0 walichopokea uwanjani Camp Nou wiki jana na kufuzu kwa fainali kwa jumla ya mabao 4-3.
Sasa Liverpool watakutana na Tottenham Hotspur ya Uingereza kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kwenye mechi ya Jumatano, Spurs walitoka nyuma na kuilima Ajax Amsterdam ya Uholanzi mabao 3-2 na hivyo kufanya matokeo kuwa 3-3 lakini wakafuzu kwa ubora wa mabao ya ugenini licha ya kwamba walilazwa 1-0 mechi ya nyumbani.
Mashabiki walishuhudia vijana Klopp wakitoka nyuma na kuandikisha ushindi huo mkubwa katika mechi ambayo kwa mara ya kwanza nyota Lionel Messi alishindwa kutekeleza kazi yake wakati alipohitajika zaidi kusaidia mabingwa hao wa La Liga ya Uhispania.
Kawaida, Barcelona humiliki mpira mara nyingi kwa lengo la kuficha makosa yao, lakini dhidi ya Liverpool walionekana kuchanganyikiwa kwa kiasi kikubwa.
Viungo wao wakiongozwa na Arturo Vidal walicheza kwa kiwango cha chini kiasi cha kumfanya Messi kuonekana kama mtu wa kawaida.
Ngome ya Liverpool chini ya ulinzi mkali wa Virgil van Dijk ilikuwa makini huku ikizuia vijana hao wa kocha Ernesto Valverde kupata bao ambalo lingeifanya mechi hiyo kuingia katika muda wa ziada kufuatia ushindi wa mkondo wa kwanza ambao Barcelona walishinda 3-0, ugani Camp Nou.
Ilivyoonekana, kikosi cha Liverpool kilikesha kikiwaza jinsi ya kuwazuia mastaa wa Barcelona huku beki huyo tegemeo alifanya kile anachofanya kila siku anapokuwa uwanjani.
Viungo wa Liverpool walitulia walipokuwa kuwanyima viungo wa Barcelona uwezo mkubwa wa kusoma mchezo, kimiliki mpira na kumpiga Messi pasi za kufunga mabao.
Liverpool waliharibu mambo mapema kwa kupata mabao ya mapema kupitia kwa Divock Origi a Georginio Wiljnaldum aliyeingia katika nafasi ya Andrew Robertson kabla ya kuanza kuvuruga wachezaji wa Barcelona kila walipokuwa na mpira.
Kijana Origi alionekana kila ilipotokea faulo, alionekana, iwe kushambulia au kuzuia na kwa kiasi kikubwa mchango wake ulichangia ushindi wao.
Kama kawaida, Liverpool ilitoa mashambuliaji yao kutoka pembeni ambako kulikuwa na Robertson na kinda Trent Alexander-Arnold ambao walicheza kwa kiwango cha juu.
Mara kwa mara mabeki wa Barcelona walipata presha wakati mpira ulikuwa karibu na eneo lao la hatari, hali ambayo ilichangia kuingia kwa mabao mawili kutokana na ulegevu wa Jordi Alba.
Juhudi za Valverde kumuondoa Vidal na kumuingiza Arthur dakika ya 75 hazikuisaidia timu yake ambayo iliendelea kushambuliwa mara kwa mara.
Lakini hatua ya kumuingiza Malcom katika nafasi ya Rakitic kulichangia kufufuka kwa kikosi chake lakini hakikufanikiwa kupata bao la kusawazisha matokeo hayo ya 4-3.
Matokeo hayo yameyeyusha kabisa matumaini ya Valverde kutwaa mataji matatu msimu huu, baada ya majuzi kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya La Liga wakati huu wanajiandaa kucheza Valencia kwenye fainali ya Copa del Rey.
Katika fainali ya UEFA, Liverpooll huenda ikacheza dhidi ya Ajax Amsterdam ama Tottenham Hotspur fainali mnamo Juni 1 jijini Madrid.