Mwanaraga wa Shujaa kusalia mkekani kwa muda mrefu baada ya jeraha
Na CHRIS ADUNGO
MWANARAGA matata wa Shujaa, Oscar Dennis, atasalia mkekani kwa kipindi kirefu kuuguza jeraha la mguu wa kulia alilopata baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Karen, Nairobi.
Licha ya hali hiyo, mwanaraga huyo wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande amejumuishwa kwenye kikosi cha nyota 29 watakaotegemewa na kocha Innocent Simiyu katika kampeni za Raga ya Dunia za msimu wa 2020-21 na Michezo ya Olimpiki ya Tokyo itakayoandaliwa nchini Japan mnamo Julai-Agosti 2021.
Mkurugenzi wa Raga katika KRU, Thomas Odundo amethibitisha kwamba familia ya Dennis kwa sasa inapanga kumsafirisha hadi Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji kwenye mguu wake uliovunjika kutokana na ajali hiyo.
Dennis aliwasili humu nchini mnamo Jumanne asubuhi kwa pamoja na wenzake watano wa Shujaa – Collins Injera, Andrew Amonde, Oscar Ouma na Willy Ambaka waliounga kikosi cha SFX10 kilichowakilisha Afrika Kusini kwenye Raga ya Dunia ya IPL World Tens nchini Bermuda.
Dennis aliwaongoza SX10 kuwapepeta Phoenix 12-0 kwenye fainali na kutwaa taji la kivumbi hicho cha World Tens Series kilichoandaliwa kati ya Oktoba 24 na Novemba 7.
Baadaya kuhusika kwenye ajali, Dennis aliyekuwa akiendesha pikipiki alikipelekwa na msamaria mwema katika Hospitali ya Aga Khan baada ya dereva wa gari lililomgonga kuhepa kwenye eneo la tukio.
“Niliarifiwa kwamba jeraha hilo lilikuwa baya. Familia imefichua azma ya kumpeleka Dennis ughaibuni kwa minajili ya tathmini zaidi,” akasema Odundo ambaye kwa niaba ya KRU, alimtakia mwanaraga huyo nafuu ya haraka.
Dennis alivalia jezi za Shujaa kwa mara ya kwanza mnamo 2018-19 katika duru za Raga ya Dunia za Hong Kong na Singapore Sevens.
Mbali na ukaguzi wa kawaida utakaolenga kubaini hali zao za afya na uwezo wa miili yao kuhimili mazoezi mazito, wanaraga wote ambao wameitwa kambini mwa Shujaa watafanyiwa vipimo vya corona kwa mujibu wa kanuni za mpya za serikali katika juhudi za kudhibiti msambao wa virusi vya corona. Vipimo hivyo vimeanza kufanyika katika uwanja wa RFUEA, Nairobi.
Kwa mujibu wa Odundo, Shujaa wanatazamiwa kuanza kujifua baada ya kupata idhini ya Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) itakayoendesha mazoezi yao katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Shirikisho la Raga Duniani (WR) tayari limefutilia mbali duru nne za kwanza za za Dubai, Cape Town, Sydney na Hamilton katika kampeni za Raga ya Dunia msimu ujao wa 2020-21. Ina maana kwamba kipute cha Raga ya Dunia katika msimu wa 2020-21 kinaweza tu kung’oa nanga mnamo Machi 2021 kwa duru za Los Angeles (Amerika) na Vancouver (Canada).
Mbali na raga ya wachezaji saba kila upande kwa wanaume, Kenya itashiriki pia fani mbalimbali katika Olimpiki za Tokyo, Japan zikiwemo mbio za marathon, voliboli (wanawake), ndondi na taekwondo (wanawake na wanaume) na kupiga mbizi au uogeleaji (wanawake na wanaume).
“Nitategemea wanaraga waliopo kwa sasa katika orodha hii ya wachezaji wa Shujaa kabla ya kuwaweka kwenye mizani kwa mujibu wa viwango tunavyovihitaji. Tutaongeza orodha hiyo baadaye kwa kuleta wanaraga wapya kwa kuwa baadhi ya wachezaji tulionao kikosini wana mikataba inayoelekea kutamatika,” akasema Simiyu.
Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mwanzoni mwa Septemba 2020 kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni.
KIKOSI CHA SHUJAA:
KCB: Andrew Amonde, Vincent Onyala, Jacob Ojee, Geoffrey Okwach, Johnstone Olindi, Levy Amunga.
Mwamba RFC: Collins Injera, Billy Odhiambo, Daniel Taabu, Tony Omondi, Mike Okello.
Impala Saracens: Sammy Oliech, Alvin Marube.
Kenya Harlequins: Willy Ambaka, Herman Humwa, Eden Agero.
Nakuru RFC: Oscar Ouma, Nelson Oyoo
Homeboyz RFC: Jeffrey Oluoch, Bush Mwale, Alvin Otieno.
Menengai Oilers: Harold Anduvate, Derrick Keyoga, Mark Kwemoi.
Kabras Sugar RFC: Daniel Sikuta, Brian Tanga.
Nondescripts: Oscar Dennis, Dennis Ombachi.
Blak Blad: Archadius Khwesa.