Michezo

Mwatate United FC yafurahia udhamini kutoka kwa Teita Estate Limited

May 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

IMEBAHATIKA kumpata mdhamini ambaye ameihami timu kwa kipindi cha miaka michache na sasa lengo la kufikia lengo lake la klabu hii ni kushiriki katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Wakati klabu za soka za hapa nchini zinapotatizika kwa kukosa udhamini, timu ya Mwatate United FC imefanikiwa kumpata mdhamini aliyeihami timu hadi kufanikiwa kushiriki kwenye Supa Ligi ya Taifa msimu ujao wa 2020-2021.

Kwa klabu ya Mwatate United FC, imekuwa ikipata udhamini kutoka kwa Teita Estate Limited kupitia kwa mkurugenzi wake Philip Kriazi ambaye udhamini wake umeifanya timu hiyo kushiriki kwenye Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza misimu mitatu kabla ya kufuzu kwa Supa Ligi ya Taifa.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, James Okoyo anasema wamepania msimu huu kuhakikisha wamefanikiwa kushinda ligi hiyo na kupanda hadi Supa Ligi ya Taifa ambayo mshindi wake hupanda hadi KPL.

“Tumepania kushinda ligi hii msimu huu ili tuweze kumridhisha mdhamini wetu Kriazi kuwa udhamini wake umeweza kufanya kazi na kuifanya timu kuendeleza juhudi zetu za kuhakikisha timu yetu imefanikiwa kufikia lengo la kushiriki ligi ya KPL,” anasema Okoyo.

Kwa wakti huu ambapo ligi hiyo imesimama kutokana na janga la Covid-19, Mwatete United iko kileleni ikiwa na pointi 34 kutokana na mechi 15 ilizocheza ikifuatiwa na MFC ambayo iko nafasi ya pili ikiwa na alama 32 baada ya kucheza mechi 16.

Baadhi ya wachezaji wa Mwatate United FC wakifanya mazoezi. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Okoyo anasema walikuwa wanasubiri kwa hamu ligi hiyo ianze kuchezwa tena lakini kutokana na janga la corona, Shirikisho la Soka Nchini Kenya (FKF) limeamua kuwapa ushindi na kupanda ngazi hadi Supa Ligi ya Taifa.

“Tutajaribu tuwezavyo kuhakikisha tunashinda Supa Ligi ambayo ni ngazi moja tu kupanda hadi ligi kuu ya KPL,” akasema kinara huyo.

Meneja wa klabu hiyo, Christopher Nyamao anasema kwa kufanikiwa lengo lao la kushinda ligi hiyo, wamefanya usajili wa wachezaji wapya saba pamoja na mkufunzi mpya ili timu iweze kuimarika na kushinda taji la ligi hiyo wanayoshiriki.

Sajili wapya wa timu huyo msimu huu ni George Onyango kutoka Eldoret Youth, Francis Ochieng (Migori Youth), Michael Otieno (Shabana), Jackim Otieno (Fortune Sacco) na wawili kutoka timu ya hapo Mwatate ya Kitivo FC, Granton Masha na Israel Mwakisaghu.

Nyamao amesema wamejaribu wawezavyo kwa misimu miwili kushinda lakini huwa wanadunda dakika za mwisho lakini ni msimu huu, wameunda kikosi ambacho kimeweza kuhakikisha kimetimiza ahadi ya kupanda hadi supaligi.

Mwatate imemsajili aliyekuwa naibu kocha wa timu ya ligi kuu ya KPL ya Chemelil Sugar, Benedict Wanjala na kumpa mamlaka yote ya wachezaji yakiwemo ya kuchukuwa wachezaji wowote wapya ambao yeye anawafikiria watasaidia kuimarisha kikosi hicho kipate ushindi.

“Tuna imani kubwa na kocha wetu mpya kuwa ataweza kuifanya timu yetu kupata mafanikio. Kocha wetu huyu amekuwa na uzoefu mkubwa kutokana na yeye kuwa anatoka timu inayoshiriki kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL),” akasema meneja huyo.

Kocha Wanjala anasema wakati huu wa tatizo la corona, amewaagiza wanasoka wake wafanye mazoezi ya mtu binafsi akiwafahamisha jinsi watafanya wakitumia simu.

“Nina imani kubwa wanagozi wangu wanafuata maagizo ninayowapa kwa njia ya simu ili mara janga la corona litakapomalizika, wawe wako fiti na tuendelee kupigania kubaki kileleni mwa ligi tunayoshiriki,” akasema mkufunzi huyo.

Mwenyekiti Okoyo ametaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ikiamua kuivunja ligi hiyo iwape kombe na nafasi ya kushiriki Supa Ligi ya Taifa msimu ujao.

La kama ligi itaendelea, Okoyo anasema wako tayari kupambana kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizobakia.

Kwa mashabiki wa timu hiyo ya Kaunti ya Taita Taveta, wana imani kubwa msimu huu timu yao inataka kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka kaunti hiyo kushiriki kwenye Supa Ligi ya taifa msimu ujao.

Timu nyingine mbili za eneo la Pwani zinazoshiriki kwenye Supa Ligi ni Modern Coast Rangers pamoja na Coast Stima ambazo kwa msimu huu zitarajie ushindani mkubwa kutoka kwa Mwatate United.

Mashabiki wa Pwani wana hamu mojawapo ya timu zao hizo kushinda ili ipande na kuwa pamoja na Bandari FC katika KPL msimu wa 2021-2022.