Nahodha wa zamani asema Gor itatinga nusu fainali CAF
NA CECIL ODONGO
NYOTA wa zamani wa Mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya(KPL) Gor Mahia, Jerry Onyango, ameeleza matumaini makubwa ya K’Ogalo kutinga awamu ya nusu fainali ya Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).
Mabingwa hao watetezi wa KPL wanajibwaga MISC Kasarani kesho kutwa kwenye mkondo wa kwanza wa kipute hicho cha CAF dhidi ya Renaissance Sportive Berkane ya Morocco iliyowasili nchini jana jioni.
Onyango ambaye alikuwa nahodha wa Gor Mahia kabla ya kustaafu soka miaka miwili iliyopita, amewataka wanasoka wa K’Ogalo kutwaa ushindi wa mabao mawili nyumbani kisha kuwabana wapinzani ugenini ili kufuzu kwa urahisi hatua ya nusu fainali.
“Kama mchezaji wa zamani, ningependa kukiri kuwa nimeridhishwa sana na umbali ambao K’Ogalo wamefika kwenye mashindano haya ya CAF. Tutafuzu kwa urahisi iwapo tutawafunga mabao mawili na kuzuia kufungwa kisha tuwadhibiti kwao kwa kuweka ulinzi imara kwenye lango letu,”
“Nafahamu kuwa itakuwa vigumu sana kuwakabili ugenini ndiyo maana lazima tuwachape hapa nyumbani. Nina imani kikosi cha sasa kinaweza kutwaa ushindi na kuwapa raha mashabiki watakaofurika uwanja wa Kasarani kushuhudia mechi hii ya kihistoria,” akasema Onyango.
Nyani huyo ambaye anafunza kikosi cha wachezaji chipukizi Gor Mahia, pia alisisitiza vijana wa kocha Hassan Oktay wana uwezo wa kuandikisha historia na kufikia makuu kwa kuiga ujasiri na ushujaa wa kikosi cha K’Ogalo kilichotwaa Kombe la Mandela mwaka wa 1987 baada ya kushinda Esperance ya Tunisia kwenye fainali.
“Kila shabiki na vizazi vya sasa vinataka K’Ogalo kuandikisha historia jinsi kilivyofanya wachezaji walioshiriki Kombe la Mandela 1987. Hilo linawezekana na nawashaajisha wasiogope chochote kwasababu hakuna nafasi ya wachezaji waoga ndani ya kambi ya Sirkal,’’ akaongeza jagina huyo.
Akigusia kukosekana kwa wachezaji tegemeo Harun Shakava, Jacques Tuyisenge, Shafik Batambuze na Ernest Wendo, jagina huyo aliwataka watakaoaminiwa kujituma vilivyo na kumdhihirishia Oktay umuhimu wao timuni.
Mnyakaji huyo vile vile ameahidi kuwa kati ya maelfu ya mashabiki watakaojaza uwanja wa Kasarani huku duru zikiarifu mabasi kadhaa yamekodishwa kuwasafirisha mashabiki kutoka eneo la Nyanza hadi Nairobi kesho.
Gor Mahia walirejea Nairobi Jumatano usiku baada ya kukita kambi eneo la Homabay na Kisumu walikojifua na kushiriki mechi za KPL dhidi ya Nzoia Sugar, Kariobangi Sharks, Zoo Kericho na SoNy Sugar.