Nairobi Water yahifadhi ufalme wa handiboli ya wanawake
Na JOHN KIMWERE
NAIROBI Water imehifadhi taji la Super Cup katika handiboli ya wanawake baada ya kutoka chini mabao 13-11 na kuzaba Ulinzi (KDF) magoli 26-22 katika fainali iliyopigiwa ugani Kaloleni Nairobi.
Nairobi Water ya kocha, Jack Herbert iliendelea kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao na kuhifadhi ubingwa huo kwa mara ya tano mfululizo. Licha ya kutoka chini kwa mabao 13-11 vipusa hao waliteremsha mechi safi na kulemea mahasimu wao.
Brenda Musambi alichangia kwa magoli saba huku Melvin Akinyi na Brenda Ariviza kila mmoja aliifungia mabao matano.
”Bila shaka napongeza wachezaji wangu kwa kuonyesha ushirikiano mwema dimbani na kuzima wapinzani wetu,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa kwa sasa wanajiandalia mechi za Ligi Kuu ambazo zimeratibiwa kukunjua jamvi mwezi ujao.
Nayo Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) ilitawazwa mfalme wa ngarambe hiyo baada ya kushinda Ulinzi (KDF) magoli 35-34 kwenye fainali ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo iliamuliwa kupitia penalti.
NCPB ilitwaa ubingwa huo baada ya kutoka nguvu sawa mara mbili mabao 25-25 na 29-29 katika muda wa kawaida na ziada mtawalia.
NCPB na Nairobi Water zilinasa tiketi ya fainali baada ya kuzoa ufanisi wa mabao 33-13 na 41-12 dhidi ya Strathmore University na NCPB mtawalia. Nao wanaume wa KDF walilaza Black Mamba mabao 23-20 wakati warembo wa KDF wakivuna mabao 28-25 dhidi ya NCPB.