Ndovu Arsenal juu ya mti tena
NA MWANGI MUIRURI
MASTAA Declan Rice na Kai Havertz walifunga mabao muhimu katika dakika za 19 na 86 mtawalia kupiga Brentford 2-1 na hivyo kupandisha ‘Ndovu’ Arsenal hadi juu ya mti wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Wenyeji Arsenal waliingia ugani Emirates mnamo Jumamosi wakiwa chini ya shinikizo za kushinda ili kujaribu kuhepa mkabano ulioko katika nafasi tatu za kwanza, timu hizo nyingine mbili zikiwa ni Liverpool na Manchester City.
Liverpool kwa sasa wana pointi 63 huku Manchester City wakiwa na pointi 62.
Arsenal wanaongoza wakiwa na pointi 64.
Liverpool na Manchester City watalipuana Jumapili ambapo wafuasi wa ‘Ndovu’ wakiomba matokeo yawe nguvu tosha ndipo Liverpool ipande hadi pointi 64 lakini wanabunduki wa Mikel Arteta wabakie kidedea kutokana na ubora wa mabao.
Nayo Man City wateremke hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 63.
Huku Arsenal wakiwa na 46 kama ubora wa mabao, Liverpool kwa sasa wana 39 huku Man City wakiwa na 35.
Askofu Danson Gichuhi almaarufu Askofu Yohana wa kutoa waumini wake wa kike mapepo, mnamo Ijumaa alikuwa ametabiri kwa unabii tosha kwamba ushindi wa Arsenal dhidi ya Brentford ulikuwa umefunuliwa wateule.
Hata sasa, Yohana anasema kwamba mwamko huu wa Arsenal haukomi hivi karibuni na utaendelea hadi sanasana, Manchester United itii kwamba jibu la swali la 2005 lililo katika wimbo wa Dry Gin na Frakaz la kutaka kujua ‘kati ya Man U na Arsenali ni gani kali?’ si swali tena.
Soma Pia: Askofu Yohana aitakia Arsenal ushindi dhidi ya Brentford
Katika mtanange huo wa Arsenal, bao la kuanza kupanda juu ya mti kwa Ndovu lilitokea dakika ya 19 lakini Yoane Wissa akasawazisha wageni katika dakika ya 45+4 hivyo basi kuwafyata midomo mashabiki wa nyumbani kwa kuteremshwa hadi nafasi ya pili lakini Havertz akawa yule mui huwa mwema katika dakika hiyo ya 86 matumaini yakiwa yamefifia.
Havertz aliyenunuliwa kutoka Chelsea amekuwa na muda mgumu mashabiki wakimfananisha na kunguru uwanjani lakini ghafla akaanza kuiva kiasi cha kuwa mwokozi.
Takwimu za mechi hiyo ya Arsenal na Brentford zilikuwa wanabunduki wakiishia kuwa na mashuti 17 dhidi ya tisa. Yaliyolenga michumani yalikiwa ni sita dhidi ya manne ya wageni.
Arsenal ilimaliza mechi hiyo ikiwa na asilimia 72 ya umiliki wa gozi nao Brentford wakiwa na asilimia 28. Wanabunduki walitandaza pasi 565 dhidi ya 221 uhakika wazo ukiwafaa Arsenal kwa asilimia 82 dhidi ya 54.