Neymar kukaa nje katika mechi tatu zijazo zitakazopigwa na PSG
Na MASHIRIKA
NYOTA Neymar Jr sasa atakosa mechi tatu zijazo zitakazopigwa na waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) baada ya kupata jeraha la paja.
Kocha Thomas Tuchel wa PSG amethibitisha kwamba fowadi huyo raia wa Brazil atakuwa mkekani hadi mwishoni mwa likizo fupi ijayo ijayo ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ambayo itapisha mechi za kimataifa katika kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Neymar ambaye ni raia wa Brazil, alipata jeraha wakati wa mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya uliowakutanisha na Istanbul Basaksehir kutoka Uturuki.
Neymar atakosa mechi ijayo ya PSG dhidi ya RB Leipzig nchini Ujerumani kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 4, 2020 kisha dhidi ya Rennes na AS Monaco kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Novemba 7 na 20 mtawalia.
“Sidhani kama ataweza pia kuchezea Brazil. Iwapo atachezea Brazil, basi itamaanisha kwamba hakuumia vibaya jinsi alivyosema, na hiyo itakuwa ishara mbaya. Tunasubiri tathmini ya madaktari hata hivyo. Ilivyo kwa sasa, naamini kwamba atarejea ugani baada ya mechi zijazo za kimataifa,” akasema Tuchel.